Leo ni Ijumaa tarehe tarehe 10 Rabi’ al-Thani, 1447 Hijria Qamaria, inayosadifiana na Oktoba 3, 2025 Miladia.
Miaka 1246 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Rabiuthani mwaka 201 Hijria, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Mussa bin Jaafar al-Kadhim (as).
Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha katika uzungumzaji, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu.
Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha (as) kuwasili Khurasan nchini Iran, Bibi Maasuma aliondoka Madina kwa lengo la kumfuata kaka yake, lakini akiwa njiani alisimama katika mji wa Qum na kufariki dunia mjini humo kutokana na maradhi au kwa mujibu wa kauli nyingine, kutokana na sumu aliyeopewa.

********************
Tarehe 10 Rabiuthani mwaka 1330 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 117 iliyopita Haramu tukufu ya Imam Ali bin Mussa Ridhaa, mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Mash’had huko kaskazini mwa Iran ilishambuliwa kwa mizinga na wavamizi wa Kirusi.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mmarekani, Morgan Shuster kuanzisha kikosi maalumu cha polisi ya Hazina Kuu ya Iran.
Urusi iliitambua hatua hiyo kuwa ni kinyume na maslahi yake haramu nchini. Mashambulizi hayo yalisababisha hasara kubwa kwa haramu ya mjukuu huyo wa Mtume (saw) na mali za thamani za eneo hilo tukufu ziliporwa na wavamizi hao.

***************
Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, wawakilishi wa Italia na utawala wa kifalme wa Austria walisaini Mkataba wa Vienna katika mji unaojulikana kwa jina hilo.
Kwa mujibu wa mkataba huo, Austria iliikabidhi Italia jimbo la Venice. Moja kati ya vipengee muhimu vya mkataba wa Vienna kilikuwa ni hiki kwamba, utawala wa kifalme wa Austria upigwe marufuku kuingilia masuala ya ndani ya Italia.
Mkataba wa Vienna ulifungua njia ya kuungana Italia mwaka 1870.

********************
Miaka 93 iliyopita katika siku kama ya leo Iraq ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza.
Iran iliiweka Iraq chini ya mamlaka yake mwaka 539 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (A.S). Iraq ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Iran hadi ardhi hiyo ilipokombolewa na Waislamu mwaka 642 Miladia.
Iraq iliendelea kudhibitiwa na utawala huo wa kifalme hadi mwishoni mwa utawala wa Bani Ummayya na mji wa Baghdad ulichaguliwa kuwa makao makuu sambamba na kuingia madarakani utawala wa Bani Abbas.

********************
Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, ilitangazwa rasmi habari ya kuungana tena Ujerumani ya Mashariki na Ujerumani ya Magharibi na nchi mbili hizo kwa mara nyingine tena zikaunda Ujerumani moja baada ya miaka 45 ya kutengana.
Baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa Ujerumani lilikaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani na lile la magharibi likadhibiwa na nchi za Magharibi.
Nchi mbili za Ujerumani ya Magharibi na ya Mashariki zilitangazwa kuasisiwa mwaka 1949 kwa kuwa na mifumo miwili tafauti ya kisiasa na kiuchumi.

***************