Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imepongeza kuanza kutekelezwa kwa mkataba mpana wa ushirikiano wa kistratejia kati ya Iran na Russia.

Katika taarifa iliyotolewa usiku wa Alhamisi, wizara hiyo imeeleza kuwa mkataba huo unaakisi dhamira ya viongozi wa mataifa hayo mawili ya kuimarisha mahusiano katika nyanja mbalimbali kwa misingi ya kuheshimiana, ujirani mwema na maslahi ya pamoja.

Alhamisi Iran na Russia zilianza rasmi utekelezaji wa mkataba huo wa miaka 20, hatua muhimu inayolenga kuimarisha uhusiano wa pande mbili. Mkataba huo ulitiwa saini na Rais wa Russia Vladimir Putin na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian mjini Moscow mnamo Januari 17, 2025.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, mkataba huo unaashiria “uamuzi wa kistratejia” uliofanywa na uongozi wa kisiasa wa mataifa hayo kwa ajili ya kuendeleza urafiki na kushirikiana katika masuala ya msingi yenye maslahi ya pamoja.

Mwezi uliopita, marais Pezeshkian na Putin walikutana mjini Tianjin, China, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), ambako walikubaliana kuongeza juhudi za kutekeleza kikamilifu mkataba huo.

Viongozi hao wawili walisisitiza kuwa mkataba huo unaweka msingi wa ushirikiano wa kina zaidi kati ya Tehran na Moscow katika sekta mbalimbali.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa kukamilika kwa mkataba huo kunaonyesha nia ya dhati ya viongozi wa mataifa hayo kwa ajili ya kuimarisha mahusiano yao katika maeneo yote yenye maslahi ya pamoja, kwa misingi ya heshima na ushirikiano.

Wizara hiyo imeeleza kuwa mkataba huo ni hatua ya kihistoria katika mahusiano ya nchi hizi mbili, na unaweza kusaidia kupanua ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo ulinzi, nishati, fedha, kilimo, sayansi na teknolojia.

Bunge la Iran liliidhinisha mkataba huo kwa kauli moja mwezi Mei, kufuatia kupitishwa kwake na bunge la Russia mwezi Aprili.

Kupitia mkataba huo, mataifa hayo mawili yamejitolea kusaidiana kukabiliana na vitisho vya kiusalama vya pamoja na kushirikiana katika masuala ya kiintelijensia.

Aidha, mkataba huo umeweka bayana kuwa iwapo taifa moja litakumbwa na shambulio, taifa jingine halitatoa msaada kwa mshambuliaji. Licha ya vikwazo vikali kutoka mataifa ya Magharibi, Iran na Russia zimezidi kuimarisha mahusiano yao katika nyanja mbalimbali kama washirika wa karibu wa kistratejia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *