Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah nchini Yemen amesema kuwa mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Ukanda wa Gaza baada ya vita ni “ramani ya Kizayuni” inayolenga kufuta haki za Wapalestina na kuimarisha udhibiti wa eneo hilo.

Abdul-Malik al-Houthi katika hotuba ya televisheni usiku wa Alhamisi amesema: “Mpango huu uliwasilishwa kwanza kwa [Waziri Mkuu wa Israel Benjamin] Netanyahu ili vipengele fulani vyongezwe na madai yote ya utawala wa Kizayuni yaweze kujumuishwa.”

Amesema kuwa mpango huo unalenga kuwanyang’anya Wapalestina haki zao, kuimarisha Israel na kugeuza eneo hilo kuwa ngome ya Kizayuni.

Kwa mujibu wa Kiongozi wa Ansarullah, mpango huo hautambui uwepo wowote wa mamlaka ya Wapalestina juu ya Gaza, na hata jina “Dola ya Palestina” halijakubaliwa—hata kwa ishara tu.

Ikulu ya Marekani ilitangaza mpango huo unaodaiwa kutaka kusitishwa kwa mapigano mara moja katika Ukanda wa Gaza, kubadilishana mateka wa Israel walioko mikononi mwa Hamas na Wapalestina walioko magerezani nchini Israel, pamoja na kuondoka Israel kutoka Gaza kwa awamu.

Katika pendekezo hilo, Hamas inatakiwa kupokonywa silaha, huku Marekani ikishirikiana na washirika wa Kiarabu na wa kimataifa kuanzisha kile kinachoitwa “jeshi la muda la kimataifa la kuleta utulivu.”

Kiongozi huyo wa Yemen amefafanua kuwa mpango huo pia unasisitiza kuwa Hamas haitakuwa na nafasi yoyote ya kuongoza Gaza. Badala yake, unapendekeza kuundwa kwa kamati ya kiutawala itakayosimamiwa na Marekani, Uingereza, na mataifa mengine, hata bila kuhusisha Mamlaka ya Palestina inayotawala Ukingo wa Magharibi.

Al Houthi ameonya kuwa: “Israel, kupitia mpango huu, inataka harakati za kupigania ukombozi wa Palestina zipokonywe silaha na kufukuzwa kwa wapiganaji kutoka Gaza. Vipengele hivi ni sehemu ya juhudi za kuigeuza Gaza kuwa eneo lisilo na nguvu za mapambano.”

Akirejelea historia ya ukoloni wa Uingereza nchini Palestina, kiongozi huyo wa Ansarullah amesema kuwa kama vile Uingereza ilivyokabidhi Palestina kwa Wazayuni, Marekani sasa inarudia mkondo huo huo.

Amesisitiza kuwa hatua ya Trump kutambua al-Quds kama “mji mkuu” wa utawala wa Israel ni miongoni mwa uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya watu wa Palestina na umma wote wa Kiislamu.

Aidha, ameonya kuwa Marekani inatafuta kuhusisha mataifa ya Kiarabu katika mradi wa kiusalama wa utawala wa Israel.

Akizungumzia msafara wa kimataifa wa meli za msaada wa Global Sumud uliokuwa unaelekea Gaza, Al Houthi amelaani hujuma ya Israel dhidi ya msafara huo na kuutaja pia kama mojawapo ya nembo kuu za mshikamano wa kimataifa na Palestina. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *