Kuanzia Ulaya, Australia na Amerika ya Kusini, mamia kwa maelfu ya waandamanaji wamejitokeza barabarani kulaani kuzuiwa kwa msafara wa Global Sumud Flotilla, uliokuwa na lengo la kuvunja mzingiro wa jeshi la Israel katika ukanda wa Gaza – eneo ambalo Umoja wa Mataifa umeonya kwamba linakabiliwa na njaa kali kufuatia karibu miaka miwili ya vita.

Msafara huo uling’oa nanga kutoka Barcelona, Uhispania mwezi uliopita, ukiwa na meli takriban 40 zilizobeba zaidi ya watu 400, wakiwemo wanasiasa na wanaharakati mashuhuri akiwemo Greta Thunberg. Licha ya juhudi zao, meli hizo zilikamatwa na kuzuiwa na jeshi la majini la Israel hata kabla ya kufika Gaza.

Kwa mujibu wa polisi wa Barcelona, takriban waandamanaji 15,000 walijitokeza katika mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Uhispania, wakiimba nyimbo za mshikamano na Wapalestina kama “Gaza, hamuko pekee yenu”, “Uhuru kwa Palestina” na “Isusie Israel.”

Polisi wa kupambana na ghasia walilazimika kuwatawanya baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuvuka vizuizi, wakitumia virungu na kuwalazimisha kurudi nyuma.

Miongoni mwa meli zilizozuiwa ilikuwa ile iliyombeba aliyekuwa meya wa Barcelona, Ada Colau, pamoja na wanaharakati wengine akiwemo Mandla Mandela, mjukuu wa Nelson Mandela. Ripoti zinaeleza kuwa huenda wakafukuzwa na Israel.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Nchini Ireland, mamia ya waandamanaji walikusanyika mbele ya bunge mjini Dublin, ambapo uungwaji mkono kwa harakati ya Wapalestina hulinganishwa na mapambano ya kihistoria ya Ireland dhidi ya ukoloni wa Uingereza.

Na nchini Ufaransa, zaidi ya waandamanaji 1,000 wamejitokeza katika uwanja maarufu wa Place de la Republique mjini Paris.

Maandamano kama hayo pia yalifanyika katika mji wa bandari wa Marseille, kusini mwa Ufaransa ambapo takriban waandamanaji 100 walikamatwa baada ya kujaribu kuzuia ofisi za kampuni ya silaha ya Eurolinks, inayotuhumiwa kwa kuuza silaha kwa Israel.

Maandamano zaidi pia yameripotiwa katika mji wa Berlin, nchini Ujerumani, The Hague Uholanzi, Tunis, Brasilia na Buenos Aires, mji mkuu wa Argentina.

Italia yatangaza mgomo Ijumaa kuunga mkono Palestina

Nchini Italia, vyama vikuu vya wafanyikazi vimetangaza mgomo wa kitaifa leo Ijumaa kuonyesha mshikamano na msafara huo wa meli wa Global Sumud Flotilla huku maelfu wakiingia barabarani kumtaka Waziri Mkuu Giorgia Meloni kuchukua msimamo thabiti kuunga mkono wanaharakati hao.

Nchini Uturuki, serikali ambayo ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa mashambulizi ya Israel, ilishuhudia msururu mrefu wa waandamanaji waliomiminika barabarani kuelekea kwenye ofisi ya ubalozi wa Israel mjini Istanbul, wakiwa na mabango yaliyosomeka “Vizuizi kamili dhidi ya uvamizi”.

Italia Rome 2025 | Maandamano ya kuonyesha mshikamano na Palestina
Wafanyakazi nchini Italia waligoma kulalamikia hali ya kibinadamu katika ukanda wa GazaPicha: Andrea Merola/ZUMA Press Wire/IMAGO

Hali kama hiyo imeripotiwa mjini Brussels, ambako takriban waandamanaji 3,000 walikusanyika mbele ya jengo la Bunge la Ulaya, wakionyesha mshikamano na Wapalestina.

Waandamanaji hao wamewahimiza viongozi wa Umoja wa Ulaya kusitisha kuipa Israel mabilioni ya fedha kupitia makubaliano ya kiuchumi na kisiasa kati ya pande hizo mbili.

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP, maandamano makubwa pia yalifanyika mjini Geneva, Uswisi, ambapo waandamanaji—wengi wao wakiwa vijana—walikusanyika karibu na kituo kikuu cha treni na kuwasha moto kama ishara ya hasira na upinzani dhidi ya hatua ya Israel kuzuia msafara wa misaada ya kibinadamu kuelekea Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *