Mjini Rabat, waandamanaji waliobeba bendera za taifa walikusanyika barabarani na kushinikiza kuimarishwa kwa sekta ya afya badala ya kupewa kipaumbele kwa ujenzi wa viwanja vya michezo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP, maandamano ya siku ya Alhamisi yalifanyika kwa amani bila kuripotiwa visa vya vurugu.

Maandamano mengine pia yameripotiwa katika miji ya Casablanca, Marrakech, na Agadir, yote yakifanyika kwa utulivu.

Hali hiyo ya kuongezeka kwa maandamano imechochewa na hasira ya umma kuhusu ukosefu wa usawa wa kijamii, hasa baada ya ripoti za mwezi uliopita kuhusu vifo vya wanawake wanne wajawazito katika hospitali ya umma mjini Agadir—tukio lililoibua maswali kuhusu ubora wa huduma za afya nchini humo.

Wengi wa waandamanaji wanaamini kuwa sekta za afya na elimu ya umma zinahitaji maboresho ya haraka, hasa wakati ambapo mamlaka zinaendelea kusukuma miradi mikubwa ya miundombinu kwa ajili ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi ujao, pamoja na Kombe la Dunia la FIFA la mwaka 2030.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *