
Vikosi katili vya Israel vinaendelea kuongeza ukatili dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, vikisababisha vifo na majeraha kwa idadi kubwa ya watu, hususan katika maeneo ya kati na kusini mwa eneo hilo.
Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza siku ya Alhamisi kuwa angalau Wapalestina 66,225 wameuawa na wengine 168,938 kujeruhiwa katika vita vya kimbari vinavyoendeshwa na Israel dhidi ya Gaza tangu Oktoba 2023.
Wizara hiyo imebaini kuwa: “Waathirika wengi bado wamekwama chini ya vifusi na barabarani huku waokoaji wakishindwa kuwafikia”.
Wengi wa waliouawa shahidi ni wanawake na watoto.
Juzi katika siku moja pekee, raia 77 waliuawa na wengine 222 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya Israel.
Shambulizi moja la utawala huo liliwaua Wapalestina wanne baada ya hema lililokuwa likiwahifadhi watu waliopoteza makazi kushambuliwa kusini mwa Deir al-Balah, katikati mwa Gaza.
Mashambulizi mengine ya anga katika Gaza ya kati na kusini yaliacha raia kadhaa, wakiwemo watoto, wakiwa wamejeruhiwa—mmoja wao akiwa katika hali mahututi.
Vifo na majeraha pia viliripotiwa kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel katika kambi ya wakimbizi ya Al-Shati mjini Gaza.
Mapema jana, Wapalestina tisa—akiwemo baba, wanawe wanne, na mjukuu wake—waliuawa katika shambulizi la anga katika eneo la Al-Mawasi, Khan Yunis, kusini mwa Gaza.
Mnamo Septemba 18, Marekani ilitumia kura ya turufu kuzuia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokuwa likitaka kusitishwa mapigano mara moja, bila masharti, na kwa njia ya kudumu katika Ukanda wa Gaza.
Azimio hilo lilitaka kuingizwa na kusambazwa kwa msaada wa kibinadamu bila vizuizi ndani ya Gaza, na kusisitiza kurejeshwa kwa huduma muhimu katikati ya baa la njaa lililothibitishwa na operesheni za kijeshi zinazozidi kuongezeka.
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, ametoa wito kwa Baraza la Usalama kushurutisha kusitishwa mapigano mara moja katika Ukanda wa Gaza, na kuhakikisha kuondolewa kwa vizuizi vyote vya Israel dhidi ya msaada wa kibinadamu, kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.