Merz ataka mwanzo mpya kwa UjerumaniMerz ataka mwanzo mpya kwa Ujerumani

Merz amesema baada ya miaka 35 ya muungano na katika nyakati ngumu kwa Ujerumani, taifa hilo linapaswa kujipanga upya na kuziangalia siku za usoni kwa ujasiri na kujiamini. Akizungumza katika hafla ya maandishimisho hayo yaliyofanyika katika mji wa Magharibi mwa Ujerumani wa Saarbrücken, Kansela Friedrich Merz alisema ni wakati wa Ujerumani kuanzisha juhudi za pamoja za muungano mpya. Amesema watu ni lazima wawe na ujasiri wa kuyakubali mabadiliko na kutokubali hofu kutawala fikra zao.

Katika hotuba hiyo Merz alikumbushia namna watu wa Ujerumani ya zamani iliyokuwa na mfumo wa kisoshalisti, walivyoyaendesha mageuzi kwa amani yaliyopelekea kuanguka kwa ukuta wa Berlin, kuungana kwa Ujerumani mbili ya Magharibi na Mashariki, hatua iliyouangusha utawala wa kidikteta wa iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani.

Kansela Merz amesema leo (03.10.2025), ni siku ya kusherehekea lakini pia akatilia mkazo kwamba siku hii inaadhimishwa wakati muhimu, wa maamauzi magumu ya kitaifa, akigusia mapinduzi ya kidijitali, miungano ya uongozi wa kiimla na uchumi wa dunia ulio na vizingiti vya kibiashara.

Ujerumani yaadhimisha miaka 35 ya muungano
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha: Oliver Dietze/epd

Ameonya kuwa mambo mengi ni lazima yabadilike endapo Ujerumani itataka maendeleo zaidi.  Friedrich Merz amewataka pia wajerumani kushikamana na kuwajibika kukabiliana na kitisho cha usalama kwa kujitolea jeshini huku akiunga mkono mageuzi yatakayoleta ustawi, teknolojia na mataifa kutoingiliana katika masuala ya ndani.

“Leo Oktoba 3, siku tunayoiadhimisha pamoja inabakia kuwa siku ya kusherehekea. Lakini lazima tujifunze kujilinda tena. Uongozi wa dunia unabadilika kwa maana ya kwamba bado hatujashuhudia kukamilika kwa vita baridi. serikali za kiimla zinatoa changamoto kwa utaratibu wa kiliberali duniani kote na kutoa changamoto kwa demokrasia ya Magharibi. Kwa hiyo ni lazima turudishe uwezo wa kutetea uhuru wetu.”

Sio ujerumani iliyoungana tu, Ulaya pia imeungana na iko imara

Kwa upande wake Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyealikwaa kama mgeni wa heshima pamoja na mkewe Brigitte katika maadhimisho hayo, amesema sio ujerumani mbili tu za Mashariki na Magharibi zilizoungana miaka 35 iliyopita, bali pia Ulaya imeungana na ipo imara.

Ujerumani yaadhimisha miaka 35 ya muungano
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Friedrich MerzPicha: Jean-Christophe Verhaegen/AFP

Hata hivyo Macron amesema licha ya amani na ustawi kuongozwa na muungano huo kila kitu kilichofanikishwa kipo hatarini akisisitiza kuwa bado kuna mivutano na mipasuko katika demokrasia za Ulaya huku akitahadharisha kwamba kilichotokea miaka 35 iliyopita kinahitaji kukumbukwa wakati wote.

Maadhimisho ya muungano pia yanafanyika wakati kukiwa na kiwingu cha kitisho cha usalama nchini Ujerumani kilichosababisha uwanja wa ndege wa Munich kufungwa kwa muda baada ya droni kuonekana angani.

Hata hivyo duru za mamlaka ya anga ya uwanja huo zimesema safari za ndege sasa zimerejea kama kawaida, baada ya awali kusimamishwa baada ya droni hizo kuonekana na kutatiza safari hizo. Kisa hiki cha hivi karibuni kinafuatia msururu wa droni kuonekana katika anga za ulaya ndani ya wiki kadhaa zilizopita na kufungua mjadala wa namna Ulaya inavyoweza kujilinda na kitisho hicho cha droni.

Tukio hilo pia limekuja siku kadhaa baada ya tamasha maarufu la bia, Oktoberfest, nchini Ujerumani mjini Munich kufungwa kwa muda kabla ya kufunguliwa tena kutokana na kitisho cha bomu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *