Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York leo kwa njia ya video kutokea Tawila, Darfur Kaskazini, baada ya kile alichokiita safari ngumu kufika huko, Brown ametoa taswira mbaya ya mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao, bei ya chakula kupanda, na ongezeko la ukatili wa kingono.
Amezisisitiza pande kinzani “Acheni vurugu, acheni vita. Tuwezesheni kupita, kusaidia waathirika.”
Mamilioni ya wakimbizi, kukwamishwa kwa msaada
Brown ameeleza kuwa takribani watu 600,000 wamekimbia hivi karibuni kutoka El Fasher na maeneo ya jirani, na kuongeza idadi ya waliofurushwa makwao hadi kudikia zaidi ya watu milioni 10 nchini kote.
“Tulilazimika kuzunguka njia ndefu, kwa sababu kuna mistari mingi ya mapambano nchini Sudan, na inakuwa vigumu sana kufika tunapohitajika,” ameeleza, akionesha changamoto kubwa zinazokabili wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.
Ameyahimiza makundi yote yenye silaha kuruhusu ufikishaji salama, wa misaada kuwafikia wenye uhitaji. Amesisitiza kuwa “Tunataka kufika kwa watu walioko mashinani.”
Mgogoro unasambaa zaidi ya Darfur
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa Darfur siyo eneo pekee lililoathirika, akisema hali pia inazidi kuwa mbaya katika maeneo ya Kordofan. “Siyo tu Darfur na El Fasher, ambako hali ni mbaya sana, bali tunakabiliwa na hali kama hiyo katika jimbo la Kordofan, ambapo njia za usambazaji misaada zimezuiliwa. Bei za chakula zinapaa juu, na fursa ya kibinadamu ni finyu sana,” amesema Bi. Brown.
Kwa soko kusambaratika na misaada kuzuiliwa, familia nyingi zinabaki bila chakula na dawa ameongeza.

UNFPA imekuwa ikiwasaidia wanawake wajawazito Darfur Magharibi kufuatia kuongezeka kwa ukosefu wa utulivu katika eneo hilo.
Ukatili wa kingono watumika kama silaha ya vita
Brown ametoa maelezo ya kutisha kuhusu ukatili wa kingono unaotumika dhidi ya raia.
Amesema “OHCHR tayari imeripoti mifumo ya ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro, unaotumika kama silaha ya vita. Hii inajumuisha ubakaji, ubakaji wa magenge, utumwa wa kingono, na ukatili wa kingono unaofikia kiwango cha mateso”.
Ameelezea hali hiyo kama “mbaya sana, akiitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuwalinda wanawake na watoto ambao ndio waathirika wakuu.
Ufadhili mdogo kuliko mahitaji
Brown ameonya kuwa ukubwa wa mgogoro unazidi uwezo wa juhudi za kibinadamu kwa sasa.
“Sudan, kama mnavyojua, ni kubwa kuliko Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania zikijumlishwa pamoja. Idadi ya watu wanaohitaji msaada ni kubwa mno, zaidi ya watu milioni 30,” amesema.
Licha ya msaada wa wafadhili, mpango wa Umoja wa Mataifa wa misaada kwa Sudan umefadhiliwa kwa asilimia 25 pekee.
“Asante kwa wafadhili wetu. Nafikiri huu ndio mpango wa misaada uliofadhiliwa zaidi, lakini bado ni asilimia 25 pekee,” ameongeza, akisisitiza kuwa bila rasilimali za haraka, mamilioni ya watu wako hatarini kutokana na njaa, magonjwa na vifo.