
Kupitia simulizi yenye nguvu kutoka kwa wanufaika, mashirika ya kiraia na watoa huduma za msaada wa kisheria, video ya UNDP inaonesha jinsi mradi wa “Amkeni Wakenya” unavyowezesha upatikanaji wa haki kwa jamii zilizotengwa na zilizo katika mazingira magumu.
Naibu Mwakilishi wa Mipango, UNDP Kenya Madalena Monojaanasema ni mtazamo wa kuvutia kuhusu uwezeshaji wa kisheria kutoka ngazi ya jamii na jukumu la ushirikiano jumuishi katika kuimarisha mifumo ya haki .
“UNDP kwa miaka mingi wamepanua sana mtazamo wetu wa upatikanaji wa haki kutoka kulenga mageuzi ya kisheria na ujenzi wa uwezo wa taasisi hadi kufanya kazi zaidi na zaidi na jamii, hasa jamii za mashinani. Haya ni masharika ya kiraia ambayo yamejikita ndani ya jamii zao, na yanaeelewa changamoto za masuala muhimu ambayo jamii zao hukabiliana nazo. Kwa hivyo, zinatetea na kuwa sauti za jamii zilizotengwa, iwe ni wanawake, watu wenye ulemavu, au vijana.”
Ubunifu wa mashinani kama vile mahakama tembezi za kaunti ya Lamu na kipindi cha redio cha Mandera vinakuwa njia za kuokoa haki kwa jamii zinazoishi pembezoni. Halima Msuo ambaye ni mnufaika Lamu anasema,
“Tunapokwenda Lamu, wanatuambia tuende hospitali mara moja kwa wiki hadi saa nne asubuhi. Yule mama aliyempoteza mume wake, alienda Lamu bila kulipia gharama zote kwa mamlaka. Sasa, nilichukua fursa hii kuja kusaidia mahakamani. Nilipewa taarifa nifungue kesi na kuwasaidia yeye pamoja na mama yake kwa mahitaji yao. Lakini kufika hapa mahakamani kunatusaidia sana. Tunashukuru. Nimepewa kesi hii, nimekuja, nikachukua cheti, na nikapata cheti. Kama mama, ninashukuru kufika katika Mahakama hii na kushiriki msaada sheria hapa Lamu Mashariki.”
Amalie Miesa ni miongoni mwa wanatoa msaada wa kisheria kwa jamii kupitia mradi huu na anasema.“Wakati nimefundishwa kutoa msaada wa sheria, wazee walikuwa hawataki kuniona nikingilia kati kesi zao.Lakini nashukuru sababu wao walipofundishwa na mimi pia nikafundishwa tukawa kitu kimoja, umuhimu ambao wanaona kwangu ni pale kwenda kukaa na kusuluisha zile kesi, si kesi za akina mama peke hata za Watoto hata za akina mama waliopigwa na wanaume zao na za mashamba huwa wananiita na wanaona umuhimu wa kuchangia pale kwa sababu mimi nimefundishwa.”
Juma Bahola Hiribae ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wazee katika eneo la Gasa huko Kaunti ya Tana pia anasema, “Tulipoangalia na kufundishwa tuliona kuna umuhimu kwa sababu ata hapo awali, kesi nyingine ni lazima tuchakue wale akina mama ambao ndio viongozi wa akina mama waje pale Gasa alafu tuanze kuwauliza,kuna hili na hili nyinyi huwa mnafanya vipi nao wanachangia kwa hiyo yalipokuja haya maneno ya kutangamana tukaona ni bora.”
Amalie Miesa ametamatisha kwa kusema, “Tofauti na zamani, kulikuwa hakuna haki lakini kupitia huu mradi na mafunzo ambayo tumepatiwa ya kutoa msaada wa sheria kuna haki inapatikana. Mimi najiskia mzuri sana sababu nimewasidia akina mama na wananipongeza. Mimi ninasikia raha sana na hii kazi natumikia bila chochote nasikia amani.”
Mpango huu wa kipekee unazingatia zaidi kuzuia ufisadi, kukumbatia matumizi ya teknolojia ya kisasa na nishati mbadala ili kurahisisha mchakato wa kisheria na kuharakisha upatikanaji wa haki.
Kwa niaba ya Muungano wa Ulaya, wanajivunia kuunga mkono mageuzi ya sekta ya haki nchini Kenya, tukijenga juu ya mafanikio ya awamu ya kwanza ya mpango huu.