Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Laila Rajab Khamis amesema iwapo akichaguliwa atamaliza tatizo la ajira, kuimarisha huduma za afya na biashara Zanzibar.

Wakati Laila akisema hayo, mgombea urais mwingine kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman yeye ameahidi kuondoa kodi kwenye bidhaa za vyakula vinavyotumika kila siku.

Laila amesema hayo leo Oktoba 3, 2025 wakati chama hicho kikizindua kampeni zake katika viwanja vya Nego Kibanda Maiti Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema licha ya kufanyika mengi na Serikali iliyopo madarakani,  lakini wanataka kufanya makubwa ikiwamo kuimarisha sekta ya afya kusomesha watoto wa Kizanzibari wawe madaktari bingwa.

“Tutawaajiri katika maeneo yao na sio tu kuwaajiri basi, lakini tutapandisha mishahara kwa asilimia 80,” amesema.

Amesema kuna tatizo kubwa na sugu la ajira, lakini baada ya NCCR kuingia madarakani watajenga viwanda vingi kuhakikisha wanamaliza kabisa tatizo hilo.

“Tunaomba mtuchague ili muone mambo makubwa tutakayofanya, baada ya kuingia madarakani,” amesema.

Amesema ndani ya siku 100 baada ya kuingia madarakani, atahakikisha wanajenga soko zuri kuliko masoko yote yaliyopo Unguja na kurejesha mikopo.

“Wakina mama huu utakuwa ndio mwisho wa kuhangaika, nitajega soko kubwa hapa Kibandamaiti ambalo halijawaji kutokea na kila mfanyabiashara atakuwa akija sokoni na gari lake mwenyewe,” amesema Laila.

Awali, mgombea mwenza wa chama hicho wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Eveline Munisi amesema lengo lao ni kuleta mageuzi katika sekta zote za Tanzania.

Munisi amesema Zanzibar ni tajiri, lakini wananchi wake hakuna wanachonufaika nacho.

“Zanzibar kuna uvuvi, lakini hakuna mnachonufaika nacho, tumekuja kuleta mageuzi tutagawa boti za kisasa kwa wavuvi wote wavue kisasa,” amesema.

Amesema chama hicho kinategemea kuweka uchumi jumuishi na suala la ajira halitakua kilio tena kwa Vijana wa kizanzibari hivyo wakimchagua Laila wa NCCR itakuwa mwisho wa yote.

OMO aahadi kuondoa kodi

Kutoka Pemba, mgombea urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema endapo akishika madaraka, utendaji wake wa kazi utawagusa maisha ya wananchi kwa kuowandolea kodi kwenye bidhaa za vyakula vinavyotumika kila siku.

Othman amesema hivi sasa vyakula bei ghali visiwani humo, kwa sababu kuna tozo na kodi zinazosababisha wananchi kushindwa kumudu kununua.

Othman ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 3,2025 akizungumza na wananchi wa Jimbo la Mtambile wilayani Mkoani, Mkoa wa Kaskazini Pemba katika mwendelezo wa kusaka kura za urais, kisiwani humo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo (Zanzibar), Omar Ali Shehe amesema Othman ndio mgombea sahihi wa urais wa visiwa hivyo, hivyo Wazanzibari wamuunge mkono Oktoba 29.

“Huyu ndie mtu sahihi atakayesimama na kuitetea Zanzibar, tunahitaji kiongozi ambaye ameyaishi maisha ya Zanzibar na huyu si mwingine ni Othman Masoud. Wazanzibari tuumpe kura zetu, huyu ndio mkombozi na tegemeo letu,”

“Othman ni mwanifu, mwadilifu, asiyekuwa na tamaa, ameshika nafasi kubwa muhimu hapa Zanzibar hamjapata kusikia ameiba au kudokoa. Ingekuwa ameiba au kudokoa basi leo redio na runinga zingeiba wimbo huo,” amesema Shehe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *