Putin amesema kutolewa kwa makombora hayo kutamaanisha Marekani imejiingiza moja kwa moja katika vita vyake na Ukraine. Ameielezea hali hiyo kuwa hatari akifafanua nguvu ya makombora hayo na uwezo wake wa kuidhuru Urusi. Rais Vladimir Putin pia amesema utoaji wa makombora hayo hautabadilisha mwelekeo wake katika uwanja wa vita lakini bila shaka utayatia doa mahusiano yake na Marekani na kufungua nafasi ya mgogoro kutanuka zaidi.
Amesisitiza kuwa Urusi sio dhaifu na iko imara katika maamuzi yake.
“Historia yetu imedhihirisha kwamba udhaifu haukubaliki, kwa sababu unajenga majaribu..Kuna fikra kwamba suala letu lolote ni lazima lisuluhishwe kwa kutumia nguvu. Nataka nisema kwamba Urusi haitaonyesha udhaifu kamwe au kutokuwa na maamuzi sahihi”
Kiongozi huyo wa Urusi amesema nchi yake itaimarisha mfumo wake wa kujikinga na makombora ili kuzuwia aina yoyote ya makombora itakayovurumishwa nchini mwake. Matamshi yake yamekuja baada ya ripoti za vyombo vya habari kwamba Marekani inafikiria kutoa makombora ya masafa marefu aina ya Tomahawk kwa Ukraine.
Ukraine: Tunataka kuimarisha ulinzi wetu dhidi ya uvamizi wa Urusi
Ukraine kwa upande wake imesema inataka kuimarisha ulinzi wake dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini mwake ulioanza takriban miaka mitatu na nusu iliyopita. Rais wa taifa hilo Volodymyr Zelensky alizungumza na rais wa Marekani Donald Trump juu ya hilo wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Huku hayo yakiarifiwa Urusi bado imeendelea na mashambulizi yake katika maeneo mbali mbali ya Ukraine. Usiku wa kuamkia leo (03.20.2025), imeshambulia miundombinu ya nishati ya taifa hilo.
Wizara ya nishati ya Ukraine imesema Urusi ilishambulia kwa droni 381 pamoja na makombora 35, ikilenga miundumbonu yake Mashariki mwa mji wa Kharkiv na katikati ya jimbo la Poltava, iliko mitambo mikubwa ya kuzalisha gesi. Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu hasara ya mashambulizi hayo katika maeneo hayo muhimu.
Mashambulizi mengine ya droni kutoka Urusi yaliyolenga Kaskazini mwa Kiev na mji wa Chernihiv yalisababisha umeme kukatika katika kinu cha nyuklia cha Chornobyl. kutokana na hilo Rais Zelensky aliishutumu Urusi kutishia usalama wa dunia kwa kukishambulia kinu hicho.
Urusi inatishia usalama wa dunia
Zelnsky alisema kila siku Urusi inalenga kurefusha vita viliopo, imekataa kutekeleza kikamilifu usitishaji wa vita na imeendelea kushambulia miundombinu ya nishati ya Ukraine ikiwemo mitambo ya nyuklia, akisema hicho moja kwa moja ni kitisho sio tu kwa Ulaya bali kwa dunia nzima.
Kwengineko uwanja wa ndege wa Munich nchini Ujerumani umefunguliwa tena na operesheni kuendelea kama kawaida. Ulifunga kwa muda kufuatia droni kuonekana angani ikiwa ni kisa cha hivi karibuni baada ya tukio kama hilo kushuhudiwa katika viwanja vya ndege vya Denmark, Norway na Poland.
Romania na Estonia zimeinyooshea Urusi kidole cha lawama ikisema imehusika na matukio hayo, madai ambao Urusi imeyakanusha vikali.