Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametoa wito wa mshikamano wa kitaifa na kutegemea imani pamoja na nguvu ya wananchi katika kukabiliana na vitisho na vikwazo, akisisitiza kuwa mauaji ya kisiasa, mashinikizo ya kijeshi na ukandamizaji wa kiuchumi haviwezi kulifanya taifa lake kusalimu amri.

Akizungumza katika mkutano na wasomi pamoja na wanaharakati wa kisiasa, kijamii na kitamaduni wa Mkoa wa Hormozgan mjini Bandar Abbas  kusini mwa nchi siku ya Alhamisi, Rais Pezeshkian aliwahimiza viongozi na raia kwa ujumla kuamini uwezo wa ndani na msaada wa wananchi ili kuendeleza juhudi licha ya changamoto.

Amesema: “Malengo ya taifa, heshima na fahari yake havipaswi kusahaulika. Tunapaswa kusimama katika mstari mmoja, kuelekea kibla kimoja, chini ya uongozi mmoja. Hii ndiyo maana ya swala ya jamaa; ni umoja. Bila umoja huu, jamaa hiyo itakuwa ganda tupu.”

Ameongeza kuwa: “Maadui wanadhani kuwa kwa mauaji ya kisiasa wanaweza kuiangusha nchi yetu, ilhali maelfu ya watu wenye sifa zaidi wako tayari kuuinua bendera hii.” Alikuwa akirejelea kampeni ya muda mrefu ya mauaji ya kisiasa dhidi ya Iran inayofanywa na Marekani, Israel, na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono nao.

Moja ya njama za hivi karibuni za mauaji ilitokea mwezi Juni, wakati utawala wa Israel ulipoanzisha shambulizi la kichokozi dhidi ya Iran, ukilenga makamanda wa juu wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia, na kuua mamia ya raia.

Rais Pezeshkian pia alizungumzia vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa kinyume cha sheria dhidi ya Iran kutokana na mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani, na kusema kuwa vikwazo hivyo haviwezi kuzuia njia ya taifa la Iran. Amebaini kuwa: “Wanaoogopa vikwazo hawaamini kuwa mtu anaweza kuendelea na safari kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na wananchi.”

Kauli hizi zimetolewa wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limerejesha vikwazo dhidi ya Iran vilivyokuwa vimeondolewa chini ya makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015. 

Rais wa Iran amekosoa jinsi maadui wa nje wanavyotumia mgawanyiko miongoni mwa Waislamu kunufaika na rasilimali za ardhi za Kiislamu kama mafuta, gesi na madini, huku wakisambaza silaha zinazochochea migogoro baina ya mataifa ya Kiislamu.

Amehimiza mazungumzo ya kikanda kwa kusema: “Kwa mataifa yote ya Kiislamu, kutoka Afghanistan na Pakistan hadi Oman na UAE, kutoka Qatar na Kuwait hadi Saudi Arabia, Iraq na Uturuki, matatizo yanapaswa kutatuliwa kwa mazungumzo, si kwa mgawanyiko na vita; adui yetu mkuu ni utawala wa Kizayuni.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *