Traoré miaka mitatu madarakani, hofu yazidi Burkina FasoTraoré miaka mitatu madarakani, hofu yazidi Burkina Faso

Miaka mitatu tangu Kapteni Ibrahim Traoré achukue madaraka kupitia mapinduzi, Burkina Faso inakabiliwa na sura mpya ya kisiasa na kijamii iliyojaa hofu na ukandamizaji.

Wakosoaji wa utawala wake wamefungwa, wengine wakilazimishwa kupelekwa mstari wa mbele kupigana na wanamgambo wa Kiislamu wenye misimamo mikali.

Akiiga mfano wa Thomas Sankara, shujaa wa mapinduzi ya Kiafrika aliyeuawa mwaka 1987, Traoré anajitambulisha kama kiongozi wa kupinga ukoloni, akisema bayana kuwa Burkina Faso“siyo demokrasia.”

Raia waliozungumza na AFP walisema hali ya ukandamizaji imeongezeka, lakini wote walitaka wasitajwe majina kwa hofu ya madhara ya kuzungumza hadharani.

“Unaweza kuzungumzia michezo au burudani tu. Ukianza siasa, kila mtu anakaa kimya,” alisema mkazi mmoja wa Ouagadougou. Hata ndani ya familia, ndugu wameanza kutiliana shaka.

Urusi | Victory Day | Siku ya Ushindi | Vladmir Putin na Ibrahim Traore Rais wa Burkina Faso
Traore amejenga usuhuba wa karibu wa Rais wa Urusi Vladmir Putin tangu alipoingia madarakani na kumfurusha mshirika wa jadi na mtawala wa kikoloni Ufaransa,Picha: picture alliance / Anadolu

Polisi wa maoni na kambi za uzalendo

Kamati za raia “watoa taarifa” zimetapakaa mitaani wakifuatilia mazungumzo na mienendo, hali inayofanya watu kuishi kwa hofu ya kuchunguzwa na jirani zao.

Zaidi ya hapo, vikosi vya jeshi la kiraia vimeanzishwa “kusafisha mitaa.” Raia waliokutwa na makosa madogo, kama kuvuka taa nyekundu, walilazimishwa kuvaa makoti maalum na kufanya usafi hadharani huku wakirekodiwa kwa televisheni.

Katika mpango wa kueneza “fikra za kizalendo,” vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 15 hulazimishwa kuhudhuria kambi za likizo zenye mafunzo ya kijeshi.

Kwa wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu, sharti kwanza wapitie kozi ya mwezi mzima ya “uzalendo,” yenye msisitizo mkubwa wa utambulisho wa kitaifa. Wachambuzi wanasema mpango huo ni jaribio la kutengeneza “raia wanajeshi.”

Mshiriki mmoja alisema: “Tulijifunza kuvuka mipaka yetu na kuweka nchi mbele ya nafsi zetu ndogo.” Lakini wakosoaji wanaona ni njia ya kuua maandamano ya baadaye.

Vyombo vya habari kimya, propaganda mtandaoni

Vyombo vya habari vya kimataifa vimetimuliwa vikishutumiwa kushirikiana na “mabeberu,” huku waandishi wa ndani wakilazimika kuwa waangalifu kupita kiasi.

“Ni vigumu leo kuhojiana na watu mitaani. Wanaogopa kushtakiwa au kutumwa mstari wa mbele kwa sababu ya maneno madogo,” alisema mwandishi mmoja wa ndani.

Kwa kuwa uhuru wa kujieleza umefunikwa, ni vigumu kupima umaarufu wa kweli wa Traoré. Lakini mitandao ya kijamii imetawaliwa na wanaharakati wa mtandaoni wanaomsifu, wengine wakiwa na mamilioni ya wafuasi.

Mwanamapinduzi Thomas Sankara

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mabango, video zinazotengenezwa kwa AI, na ujumbe wa kupinga mataifa ya magharibi hutawala mtandaoni, ukimuonyesha Traoré kama “shujaa anayesimama dhidi ya njama za kimataifa.”

Hata hivyo, ahadi yake ya kurejesha usalama haijakidhi matarajio. Ingawa anadai jeshi limekomboa zaidi ya asilimia 72 ya nchi, wachambuzi wanasema makundi ya Al-Qaeda na IS bado yanadhibiti maeneo makubwa, huku serikali ikitisha raia mijini na wanajihadi wakitisha vijijini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *