Chini ya mashambulizi yasiyokoma, shule, hospitali, na makazi ya dharura  vimekuwa walengwa, na kuacha wakazi wakiwa hatarini zaidi.

Madhara kwa raia yamefurutu ada

“Mwaka huu, kumekuwa na mashambulizi makali kando ya mstari wa mbele wa mapambano, na mashambulizi makubwa ya anga, hasa katika maeneo yenye wakazi wengi. Katika baadhi ya miji ya mstari wa mbele, karibu nyumba zote zimeharibiwa au kuangukiwa na makombora,” amesema Kamisha huyo Mkuu wa Haki za Binadamu Volker Türk mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Amebainisha kuwa shambulio la Septemba 6, mamlaka za Urusi zilitumia mabomu 823, ikiwa ni pamoja na Ndege zisizo na rubani au droni 810 za muda mrefu na misumari 13, akilielezea kama “shambulio kubwa zaidi la anga katika vita hii.”

Idadi ya vifo inaongezeka sanjari na hatari

Kulingana na Umoja wa Mataifa, idadi ya raia waliopoteza maisha au kujeruhiwa katika miezi minane ya mwanzo wa mwaka huu wa 2025 imeongezeka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na 2024, na mwezi wa Julai meaashiria kuwa mwezi hatari zaidi katika zaidi ya miaka mitatu.

“Tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Shirikisho la Urusi, tumeorodhesha raia zaidi ya 50,000 wa Ukraine waliouawa au kujeruhiwa, ikiwa ni pamoja na watoto zaidi ya elfu tatu,” amesema Bwana Türk.

Ameongeza kuwa mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu, vituo vya umeme, miundombinu ya gesi, madaraja, na reli yamepunguza uweo wa maisha ya kila siku, huku makundi dhaifu yakiathirika zaidi.

Kashfa za kuteswa na kuwekwa gereza bila sababu
Mkuu wa Haki za Binadamu pia amekosoa ukiukaji wa mfumo wa sheria dhidi ya wafungwa. “Tumeorodhesha mauaji ya kiholela 90 ya raia wa Ukraine waliokuwa wamekamatwa na mamlaka ya Urusi,” amesema Türk, akibainisha vifo 38 gerezani vilitokana na mateso, ukosefu wa huduma za afya, au hali mbaya.

Ameongeza kwamba marekebisho ya sheria za Urusi yameunda mfumo unaowapa askari uhuru wa kutochukuliwa hatua, na hivyo ukiukaji kama huu hauadhibuwi.

Mamlaka ya Ukraine, ingawa pia imehusishwa na ukiukaji fulani wa haki, imedhaniwa kuchukua hatua za kuboresha kinga za wafungwa.

Changamoto katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi

Türk aliripoti kwamba wakazi katika maeneo yanayoshikiliwa na Urusi wanakabiliwa na shinikizo la kupata uraia wa Urusi ili kupata huduma za msingi au hatari ya kuonewa na kupelekwa kigeni.

Shule sasa zinafuata mtaala wa Urusi unaosisitiza elimu ya kiutamaduni na kijeshi, huku ufuatiliaji na vikwazo vikiimarishwa. “Mara nyingi, hatua hizi zinaonesha jitihada za makusudi za kuzuia upinzani na utambulisho wa Kiukraine,” amesema.

Wito wa kuwajibika na kumaliza vita

Türk amesema “Ninaomba Shirikisho la Urusi “lisitekeleze mauaji ya kiholela, mateso, unyanyasaji, na ukatili wa kijinsia dhidi ya raia waliokamatwa na wafungwa wa vita,” amesema .

Alisisitiza pia kwamba Ukraine iheshimu sheria za kimataifa na pande zote zichukue hatua za uhakika za uchunguzi huru na kuhakikisha kwamba wahalifu wanawajibishwa.

“Vita hivi vinahitaji kumalizika. Madhara kwa raia, na kwa wanajeshi na familia zao, ni makubwa na ya kuumiza moyo,” amesema, akionya kwamba ghasia hizi zinaendelea kuwa tishio la kuenea zaidi ya mipaka ya Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *