Wananchi Waislamu wa Iran wamefanya marasimu ya kumbukumbu ya mwaka mmoja ya kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.

Wananchi kote Iran jana Alkhamisi walishiriki katika hafla hizo za kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuuawa shahidi Hassan Nasrallah na viongozi wengine wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon.

Wananchi wa Iran wameadhimisha kumbukizi hiyo ya kuuawa kiongozi huyo wa mrengo wa Muqawama katika eneo la Asia Maghaibi kwa maandamano, marasimu, vikao na mikusanyiko ya dua.

Mmoja wa Wairani waliohudhuria maadhimisho hayo amesema, “Tunasimama kwa heshima na taadhima kwa ajili ya kujitolea kwake (Nasrullah) muhanga, na vile vile wanamapambano wenzake, ambao walisimama na Palestina, wakaitetea, na kulipa gharama kubwa kwa ajili yake.” 

Hafla kubwa ilifanyika katika medani ya Imam Hossein hapa mjini Tehran, ambapo idadi kubwa ya watu na maafisa wa serikali na kijeshi walihudhuria.

Hafla kama hizo zilifanyika katika miji mbali mbali kote Iran siku ya Alkhamisi. Wanachi katika nchi kadhaa za Waislamu wamewaenzi na kuwaomboleza Sayyid Hassan Nasrullah na Mkuu wa zamani wa Baraza la Utendaji la harakati hiyo, Sayyid Hashem Safieddine, waliouawa shahidi katika shambulio la anga la Israel huko Beirut mwaka jana.

Sayyid Nasrullah aliuawa shahidi katika shambulizi kubwa la anga la Israel kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut mnamo Septemba 27, 2024, wakati jeshi la Kizayuni liliposhadidisha kampeni yake dhidi ya Hizbullah. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *