Takriban watu 29 waliuawa kwa risasi za jeshi la Israeli kusini mwa Ukanga wa Gaza. Kwa mujibu wa maafisa wa Hospitali ya Nasser ni kwamba watu 14 kati yao waliuawa katika kitengo cha jeshi la Israeli.
Katika mji wa kati wa Deir al-Balah, maafisa wa Hospitali ya Al-Aqsa wamesema walipokea miili ya watu 16 waliouawa katika mashambulizi ya Israeli. Kwa upande wake shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF limeripoti kuwa mtaalamu wake wa tiba aliuawa wakati akisubiri basi huko Deir al-Balah, katika shambulio lililowajeruhi vibaya watu wengine wanne.
Daktari Muhammad Al-Mahrouq, naibu mkuu wa idara ya tiba ya viungo kwenye hospitali ya Al-Aqsa amesema hospitali hiyo imezidiwa na wagonjwa.
“Changamoto tunazokabiliana nazo kwa sasa ni ukosefu wa vifaa na rasilimali, pamoja na idadi kubwa ya wagonjwa na msongamano, jambo linalotufanya tushindwe kutoa huduma bora kadri ya uwezo wetu”, alisema Al-Mahrouq.
Hali mbaya ya kina mama na watoto
Hospitali nyingine ziliripoti vifo vingine kadhaa kutokana na mashambulizi ya Israeli. Hakukuwa na tamko la haraka kutoka kwa jeshi la Israeli, ambalo husema linawalenga wapiganaji tu na kulilaumu kundi la Hamas kwa kuhatarisha raia kwa kuendesha shughuli zake katika maeneo yenye watu wengi.
Huko mjini Geneva, shirika la watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, limesema Ijumaa (03.10.2025) kwamba akina mama na watoto wachanga huko Gaza wanakabiliwa na hali mbaya sana, wakati Hospitali ya Nasser iliyoko kusini mwa ukanda huo imezidiwa na wagonjwa wanaokimbia kutoka kaskazini.
Hamas bado yahitaji muda kuchambua mpango wa Trump
Huku hayo yakijiri, afisa mmoja wa kundi la Hamas aliliambia shirika la habari la AFP Ijumaa (03.10.2025) kwamba kundi hilo bado linahitaji muda wa kuchunguza mpango uliotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump wa kumaliza vita vya Gaza. Afisa huyo ambaye hakutana jina lake litajwe amesema Hamas bado inaendelea na mashauriano kuhusu mpango wa Trump. Kwa upande wake Mohammad Nazzal, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, amesema kwamba mpango huo wa amani una vipengele vinavyotia wasiwasi.
Wakati huo huo, Israel imezuia sehemu kubwa ya meli zaidi ya 40 zilizokuwa kwenye msafara wa misaada uliokuwa ukifuatiliwa kwa karibu, uliobeba misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema kwamba wanaharakati waliokuwa ndani ya meli hizo — wakiwemo Greta Thunberg na wabunge kadhaa wa Ulaya — wako salama na wanapelekwa Israel kuanza “taratibu” za kuwarejesha makwao.
Vyanzo : AP, AFP