
Takriban watu 14 wameuawa siku ya Alhamisi katika shambulizi lililofanywa na makundi ya wanamgambo dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani katika jimbo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani.
Shambulizi hilo lilitokea katika eneo la Djugu asubuhi, wakati wakimbizi kutoka kambi ya Rhoo walipokuwa wakielekea kwenye mashamba katika vijiji vya jirani.
Radio ya Umoja wa Mataifa, ikinukuu mashuhuda, imeeleza kuwa waathirika wengi walikuwa wakulima, na ikahusisha shambulizi hilo na kundi la wanamgambo la Cooperative for the Development of Congo (CODECO).
Taarifa imesema walioshuhudia waliripoti kuwa wanamgambo waliwateka, wakafyatua risasi na kuwakatakata baadhi ya waathirika kwa visu. Idadi ya vifo bado ni ya muda kutokana na ugumu wa kufika eneo hilo.
Hakukuwa na tamko rasmi kuhusu tukio hilo hadi sasa.
Hata hivyo, baada ya shambulizi hilo, hofu kubwa ilitanda katika kambi ya Rhoo, ambayo inahifadhi maelfu ya wakimbizi wa ndani.
Viongozi wa jamii za kiraia wa eneo hilo wametoa wito wa haraka kwa jeshi kuingilia kati na kulinda usalama wa eneo hilo.
DRC imekuwa ikikumbwa na mojawapo ya migogoro mirefu na tata zaidi duniani, yenye mzozo mkubwa wa kibinadamu, ambapo watu milioni saba wamefurushwa makwao. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Makundi ya wanamgambo na waasi yanaendelea kuwatisha raia katika maeneo ya mashariki mwa DRC. Umoja wa Mataifa uliripoti kuwa mwezi Julai mashambulizi ya kikatili yalifanywa na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF), pamoja na makundi ya CODECO na Raia Mutomboki/Wazalendo katika maeneo ya Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.
Eneo hilo la mashariki mwa DRC lina utajiri mkubwa wa madini nadra ambayo ni muhimu katika vifaa vya kiteknolojia na hivyo madola ya Magharibi yanatuhumiwa kuchochea vita eneo hilo ili kuendelea kupora utajiri wa madini.