
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, kitongoji cha Daraga Oula kilichopo magharibi mwa El-Fasher kimekuwa kikilengwa mara kwa mara na mashambulizi ya RSF, yakihusisha matumizi ya mabomu, droni, na uvamizi wa ardhini kati ya Septemba 19 hadi 29.
Katika tukio la hivi karibuni lililolenga makaazi ya raia, RSF ilirusha kombora lililosababisha vifo vya watu 16, wakiwemo wanawake watatu, na kuwajeruhi wengine 21, wakiwemo watoto watano. Mtandao wa madaktari wa Sudan umetaja tukio hilo kama “mauaji ya kimbari.”
Vita kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF vilianza mnamo mwaka 2023 baada ya mivutano kuzuka kati ya washirika hao wa zamani waliotarajiwa kusimamia kipindi cha mpito kuelekea demokrasia baada ya mapinduzi ya mwaka 2019.
Hali ya kibinadamu katika mji wa El-Fasher na maeneo ya Darfur inaendelea kuwa mbaya, huku mashirika ya kimataifa yakihimiza hatua za haraka kuchukuliwa ili kuwalinda raia na kusitisha mapigano.