Unguja. Mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman ameahidi kufanya mageuzi katika utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wanaoishi katika visiwa vidogo vilivyopo Zanzibar.

Amesema katika utendaji wake, atahakikisha Serikali inamfanya kila Mzanzibari awe anahisi kuwa sehemu ya nchi bila kujali umbali alipo.

Othman amesema hayo leo, Oktoba 4, 2025 alipowasili  Kisiwa cha Fundo, wilayani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema kisiwa hicho, chenye wakazi 1,200 kimekuwa miongoni mwa maeneo ambayo kwa muda mrefu yanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii.

Kwa mujibu wa Othman, Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuvithamini visiwa vidogo licha ya mchango mkubwa wanaoutoa kupitia sekta ya uvuvi.

Amesema Serikali atakayoiongoza, atahakikisha wananchi wote wanaoishi kwenye visiwa wanapata huduma stahiki kama ilivyo kwa wananchi wanaoishi mijini.

Amebainisha Serikali itaweka mifumo bora ya kuimarisha sekta ya uvuvi, ikiwa ni pamoja na kuwapatia wavuvi boti za kisasa zitakazowawezesha kufika katika kina kirefu cha bahari kwa usalama zaidi, sambamba na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi na kusindika samaki.

Ameahidi kuboresha huduma za afya, hasa za uzazi kwa wajawazito, ambazo zimekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Fundo na visiwa jirani.

Othman ameeleza ni aibu kuona wajawazito wakipoteza maisha kwa kukosa huduma za haraka, hivyo Serikali yake itahakikisha zahanati za kisasa zinajengwa katika kila kisiwa, zikiwa na madaktari na vifaa vya kisasa.

Amesema ataunda mifumo ya elimu inayozingatia mazingira ya bahari na uvuvi ili kuwapa vijana wa visiwani ujuzi wa kujiajiri na kuchochea uchumi wa maeneo yao.

Kwa upande wa vijana amesema wana uwezo mkubwa wa kubadili maisha yao, wanachohitaji ni mazingira bora ya kujifunza na kufanya kazi.

Mkazi wa Fundo, Khamis Salim amesema ahadi za Othman ni matumaini kwao na kwamba, kwa muda mrefu wamekuwa wakisahaulika.

Amesema wameguswa na ahadi zake na wako tayari kumpa kura ifikapo siku ya uchaguzi.

“Tumepata matumaini makubwa. Tumemsikiliza kwa makini na tumeona anajua matatizo ya watu wa visiwani. Sisi wazee wa Fundo tumeamua, kura zetu zote ni za Othman Masoud,” amesema.

Mwanakhamis Abdalla amesema wananchi wa Fundo wanataka kiongozi atakayewakumbuka baada ya uchaguzi, siyo kuja na ahadi zisizotekelezeka.

Amesema wameamini Othman ni kiongozi mwenye nia njema kwa wanyonge.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *