Magaidi sita wanaohusishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel wamenyongwa nchini Iran mapema leo Jumamosi.

Shirika la habari la Mehr limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, magaidi hao wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi unaotaka kujitenga na wenye uhusiano na utawala wa Kizayuni wamenyongwa Jumamosi asubuhi huko Khuzestan, kusini magharibi mwa Iran.

Magaidi hao walikuwa wamekiri kuhusika na vitendo kadhaa vya ukatili, yakiwemo mauaji ya maafisa wanne wa usalama na shambulio la bomu huko Khorramshahr.

Aidha walihusika na mashambulizi ya silaha kwenye benki, kurusha guruneti kwenye kituo cha kijeshi na kufyatua ovyo risasi misikitini,” shirika hilo la habari limesema.

Sheria ya ujasusi inaweka adhabu kali zaidi kwa wale wanaojihusisha na shughuli za kijasusi au wanaoshirikiana na utawala wa Kizayuni na serikali zenye uadui dhidi ya usalama na maslahi ya taifa la Iran. 

Hivi karibuni pia, Idara ya Mahakama ya Iran ilitangaza habari ya kunyongwa majasusi watatu wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika jela ya Urmia kaskazini magharibi mwa Iran.

Aidha mwishoni mwa Agosti mwaka huu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) lilitangaza kukamatwa kwa mtandao wa kigaidi unaohusishwa na shirika la ujasusi la Israel, Mossad, katika mkoa wa Khorasan Razavi. Majasusi hao walihusika katika shughuli za ujasusi na hujuma ndani ya Iran wakati wa mashambulizi ya siku 12 yaliyofanywa na Israel dhidi ya taifa hili mwezi Juni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *