Chombo komoja cha habari cha utawala wa Kizayuni kimedai kuwa jeshi la Israel limeamuru kupunguzwa operesheni za kijeshi huko Ghaza baada ya Hamas kukubali kwa masharti mpango wa nukta 20 wa Donald Trump kuhusu kusimamishwa vita kwenye ukanda huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars – Redio ya jeshi la Israel imedai mapema leo Jumamosi kwamba majeshi ya Israel yameamriwa kupunguza shughuli zao katika Ukanda wa Ghaza hadi “kiwango cha chini” na kutofanya shambulio lolote isipokuwa kwa ajili ya kujilinda. Kwa mujibu wa redio hiyo, agizo hilo limetolewa huku operesheni ya “kuuteka mji wa Ghaza” ikiwa nayo imesitishwa.
Kauli hiyo imetolewa saa chache baada ya Harakati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas kukubali kwa masharti mpango wa rais wa Marekani Donald Trump wenye vipengele 20 wa “amani huko Ghaza”.
Katika ujumbe wake kwenye Twitter, Trump amesema kuwa, majibu hayo ya Hamas ni kuonesha harakati hiyo iko tayari kwa ajili ya “amani ya kudumu” na ameiamrisha Israel isitishe mara moja mashambulizi yake huko Ghaza.

Kabla ya hapo na katika kujibu mpango wa kusitisha mapigano wa Donald Trump, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ilikuwa imetangaza kukubali kukomesha kabisa vita, mabadilishano ya mateka na kutaka kuangaliwa upya mustakabali wa Ghaza kwa kuzingatia maslahi mapana ya kitaifa ya Palestina.
Kwa mujibu wa Al-Alam, harakati hiyo imetoa taarifa na kutangaza kwamba jibu hilo la masharti limetolewa baada ya mashauriano ya kina ya ndani ya HAMAS na baina ya makundi ya Wapalestina na wapatanishi wa kieneo.
Katika taarifa hiyo, Hamas, imetilia mkazo wajibu wake wa kitaifa na haja ya kusimamishwa mara moja jinai na mauaji ya umati yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina.
Hamas imeshukuru juhudi za nchi za Kiarabu, za Kiislamu na za kimataifa za kuilazimisha Israel kusimamisha vita, kubadilishana wafungwa, kuruhusu kuingia mara moja misaada ya kibinadamu huko Ghaza, kupinga kukaliwa kwa mabavu Ghaza na kupinga kulazimishwa kuhama watu wa Palestina.
HAMAS imesema: Katika kalibu ya makubaliano ya kusitisha kikamilifu vita na kuondoka wanajeshi wanaoyakalia kwa mabavu maeneo ya Ghaza, HAMAS nayo kwa upande wake inakubali kuwaachilia huru mateka wote wa utawala wa Kizayuni walio hai na waliokufa kwa msingi uliopendekezwa na Trump.