Katika kuendelea sera za undumakuwili za kundi la G-7 mkabala wa Iran; kundi hilo limedai kuwa linataka kuendeleza diplomasia mkabala wa kadhia ya nyuklia ya Iran.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za G-7 wamesisitiza kuhusu kuendelea kutumia diplomasia katika kadhia ya nyuklia ya Iran na kutaka kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington. Kundi hilo Jumatano iliyopita lilitoa taarifa na kutangaza kuwa: Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la G7 linalozijumuisha Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza, Marekani na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya wako pamoja katika kuunga mkono kuhuishwa utararibu wa Snapback yaani hatua iliyotekelezwa na Troika ya Ulaya ya kuirejeshea Iran vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na vikwazo vingine. Taarifa hiyo imedai kuwa, hatua hiyo ni matokeo ya kushindwa mtawalia Iran kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G-7 walisema hivi na hapa ninanukuu: ” Tunaunga mkono kurejeshwa utekelezaji wa maazimio yote yaliyokuwa yameondolewa huko nyuma,”mwisho wa kunukuu.

Taarifa ya G-7 imedai kuwa: Diplomasia ni suala la dharura hivi sasa ambapo mchakato wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umepelekea kurejeshwa vikwazo hivi tajwa. Tunaitaka Iran ijiepushe na hatua yoyote ya kuibua mivutano, ianze mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani haraka iwezekanavyo, na ichukue hatua zinaoonekana kuelekea kutekeleza kikamilifu ahadi zake kuhusu kutoeneza silaha za nyuklia.
Taarifa ya G-7 imeongeza kuwa: Iran inapasa kushirikiana kikamilifu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) bila kuchelewa zaidi na kutekeleza kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa Makubaliano ya NPT. Hii ni pamoja na kuuruhusu wakala wa IAEA kuanza tena kukagua vituo vya nyuklia vya Iran na kutoa ripoti kuhusu mada zote za nyuklia inazomiliki ikiwa ni pamoja na akiba ya urani iliyorutubishwa pakubwa ambayo haiwezi kuhalalishwa kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Tutaendelea kushirikiana na pande zote ili kufikia ufumbuzi wa kidiplomasia utakaotoa hakikisho kwamba Iran kamwe haitamiliki silaha za nyuklia.
Taarifa ya G7 kwa mara nyingine tena inadhihirisha wazi sera za undumakuwili za nchi za Magharibi mkabala wa kadhia ya nyuklia ya Iran. Troika ya Ulaya bila sababu yoyote yenye mashiko inadai kuwa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vimetekelezwa kwa mara nyingine tena; na kwamba inataka kuzingatiwa pakubwa vikwazo hivyo na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa, lakini wakati huo huo nchi izo tatu za Ulaya zinadai kutaka kuendeleza diplomasia kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran. Kwa hakika, nchi wanachama wa G-7 zinazoongozwa na Marekani kwa wakati mmoja zinastafidi na wenzo wa mashinikizo na kutaka kufanyika mazungumzo. Lengo la nchi za Magharibi si kufikia makubaliano ya msingi na ya kimantiki na kwa mujibu wa maslahi ya pande mbili na Iran, bali mazungumzo yanayokusudiwa na G-7 ni Iran kutegea sikio na kukubali bila masharti matakwa yote ya kujitanua ya nchi za Magharibi ambayo sasa hata yamevuka pia kadhia ya nyuklia; na kama alivyobainisha Marco Rubio Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, nchi za Magharibi zimetaka kuwekewa vizuizi kikamilifu uwezo wa makombora wa Iran.
Ni wazi kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imesimama kidete na kukabiliana na dhulma na hatua za kujitanua za Marekani na washirika wake wa Ulaya haiko tayari kukubali hatua hizi za kijuba na zisizo na kimantiki zilizojengeka juu ya msingi wa mabavu na uonevu.
Suala jingine ni madai ya kushangaza ya Troika ya Ulaya na kisingizio chake kwa ajili ya kuhuisha utaratibu wa Snapback yaani eti Iran imekiuka pakubwa makubaliano ya JCPOA. Iran iliendelea kutekeleza ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA kwa takriban mwaka mmoja na nusu baada ya Marekani kujiondoa kinyume cha sheria na kwa upande mmoja katika makubaliano hayo mwezi Mei 2018 katika muhula wa kwanza wa urais wa Donald Trump na kwa kuzingatia kauli za nchi za Ulaya eti kwa ajili ya kufidia taathira za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani mkabala wa kampeni ya mashinikizo ya juu zaidi; na hatimaye Iran ilipunguza majukumu yake hatua kwa hatua kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA baada ya Umoja wa Ulaya na Troika ya Umoja huo kushindwa kutekeleza majukumu na ahadi walizotoa. Nchi za Ulaya hazikuwa tayari pia kutekeleza ahadi zao zozote ndani ya JCPOA, bali ziliamua kuunga mkono pakubwa kampeni ya vikwazo dhidi ya Iran.
Esmail Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran pia ameashiria katika ujumbe aliotuma katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kuhusu barua iliyotumwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa E3 kuhusu kuwa kinyume cha sheria hatua ya Troika ya Ulaya na Marekani ya kurejesha maazimio ya Baraza la Usalama yaliyokwisha muda wake na kuandika: Hatua ya nchi 6 kati ya 15 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kutouunga mkono kurejeshwa maazimio hayo yaliyokuwa yameondolewa inaonyesha mgawanyiko wa wazi ndani ya Baraza la Usalama juu ya suala hili. Ni dhahir shahir kuwa karibu nusu ya Baraza la Usalama, ikiwa ni pamoja na wanachama wawili wa kudumu, hawaamini kwamba kuiwekea tena Iran vikwazo ni hatua halali na iliyostahiki.
