Maandamano yanaendelea nchini Morocco, kushinikiza mageuzi kuhusu namna huduma zinavyotolewa kwa wananchi, lakini pia kumaliza visa vya ufisadi.

Makabiliano makali yanaripotiwa kutokea baina ya waandamanaji na vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Vijana hao wameunda vuguvugu na kuliipa jina GenZ 212, kupanga maandamano ya amani kulalamikia changamoto mbalimbali zinazotokea kwenye taifa hilo la Afrika Kaskazini, likiwemo pia mageuzi kwenye sekta ya afya na elimu lakini pia kusitishw ubaguzi dhidi vijana na wanawake. Siku ya Jumatano mauaji ya Kwanza, yalishuhudiwa, baada ya waandamaji kupigwa risasi na kuuawa, kwa madai ya kushambulia kituo cha polisi katika mji wa Agadir.

Maandamano hayo yalianzia huko Agadir kutokana na hali mbaya na huduma mbovu katika hospitali za umma, na kuenea haraka kupitia mitandao ya kijamii hadi miji mingine ya nchi. Kwa mujiibu wa Chama cha Haki za Kibinadamu cha Morocco, kama ilivyotajwa na shirika la habari la Associated Press, zaidi ya watu 120 wamezuiliwa tangu maandamano hayo yaanze. Waziri Mkuu wa Morocco, Aziz Akhannouch, ambaye pia anahudumu kama Meya wa Agadir, ametetea rekodi ya serikali yake, akisema maandamano hayo yamechochewa kisiasa.

Maandamano kama hayo yanayoongozwa na vijana yametikisa nchi nyingine duniani katika miaka na miezi ya hivi karibuni. Nchini Madagascar, maandamano kuhusu uhaba wa umeme na maji yalisababisha kuvunjwa kwa serikali siku ya Jumatatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *