Trump ametoa amri ya kiutendaji akidai kuwa shambulio lolote katika ardhi ya Qatar litahesabiwa kuwa tishio la usalama kwa Marekani.
Rais Donald Trump wa Marekani ametia saini amri mpya ya utendaji ambayo inasema kuwa shambulio lolote katika ardhi ya Qatar litachukuliwa kuwa tishio la usalama kwa Marekani.
Ikiwa kama sehemu ya mpango wa kumaliza vita huko Gaza na kufidia Qatar kufuatia shambulio la utawala wa Israel dhidi ya Doha, Trump alitia saini amri hiyo siku ya Jumatatu ambayo inainua kiwango cha kujitolea Washington kwa ajili ya kudhamini usalama wa Qatar. Kwa mujibu wa tovuti ya Axios, haya ni makubaliano ya usalama ambayo hayajawahi kutokea tena kati ya Marekani na nchi yoyote ya Kiarabu.
Kwa mujibu wa amri hiyo iliyochapishwa rasmi Jumatano, Oktoba 1, Marekani itachukulia shambulio lolote la silaha kwenye ardhi, mamlaka au miundombinu muhimu ya Qatar kama tishio kwa amani na usalama wake yenyewe.
Habari hii ilitangazwa wakati Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, alipokutana na Trump katika Ikulu ya White House, ambapo pia inadaiwa alimshinikiza amuombe radhi Amir wa Qatar kwa njia ya simu kutokana na shambulio la anga la utawala huo huko Doha na kulengwa makazi ya viongozi wa harakati ya Hamas.
Kuhusu chanzo cha kutolewa uamuzi huo wa Trump, ambapo imedaiwa kuwa shambulio lolote la silaha katika ardhi ya Qatar litachukuliwa kuwa tishio kwa usalama wa taifa la Marekani, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:
– Qatar ni mwenyeji wa kambi ya anga ya “Al-Udaid”, ambayo inachukuliwa kuwa kituo kikubwa zaidi cha kijeshi cha Marekani katika ukanda huu na ina jukumu muhimu katika harakati za kijeshi za Washington katika eneo la Asia Magharibi na hata kwingineko. Hivyo ni wazi kuwa shambulio lolote dhidi ya nchi hii linaweza kuhatarisha usalama wa vikosi vya Marekani.

– Nafasi ya Qatar katika mazungumzo ya amani ya Gaza na mawasiliano na makundi ya Wapalestina imeifanya kuwa mhusika mkuu katika siasa za Mashariki ya Kati.
– Ushirikiano wa kiusalama na kijasusi: Qatar ina jukumu muhimu katika kubadilishana taarifa za usalama na Marekani, hasa katika uwanja wa kukabiliana na ugaidi.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba utawala wa Trump unaweza kutumia vitisho dhidi ya Qatar kama chombo cha kuimarisha uwepo wake wa kijeshi au kushinikiza wahusika wengine wa kikanda, bila kukusudia kuitetea Qatar.
Jambo muhimu kuhusu madai mapya ya Trump kwamba shambulio lolote la silaha katika ardhi ya Qatar litahesabiwa kuwa tishio kwa usalama wa taifa wa Marekani ni kwamba amri yake ya kiutendaji katika suala hili inakuja baada ya Israel kufanya shambulio la kutaka kuwaua viongozi Hamas, hatua ambayo ilichukuliwa kwa ushirikiano wa wazi wa Trump mwenyewe. Madai kwamba utawala wa Trump, ulijulishwa kuhusu shambulio hilo katika dakika za mwisho kabisa, ni uwongo mtupu, kwa kutilia maanani kuwa Marekani ina mitambo na mifumo mbali mbali ya rada na upelelezi huko Qatar na nchi nyingine jirani ambayo inaweza kugundua kirahisi harakati zozote za ndege za kivita za Israel kabla hazijafanya shambulio la kijeshi.
Kama Trump alikuwa mkweli kuhusu dhamira yake ya kulinda usalama wa Qatar, angeweza kumuonya Netanyahu na kumzuia kuishambulia nchi hiyo ya Kiarabu. Hivyo ni wazi kuwa Marekani haipingi na hata imeridhishwa na juhudi za Israel za kutaka kuwaua viongozi wa Hamas huko Qatar. Hili linathibitishwa wazi na matamshi ya Karoline Leavitt, msemaji wa utawala wa Donald Trump, aliyesema Jumanne, Septemba 9, bila kulaani shambulio la Israel huko Qatar kwamba, kuondolewa Hamas, ambayo eti imenufaika na mateso ya wakaazi wa Gaza, ni “lengo lenye thamani.”
Inaonekana kwamba madhumuni ya Trump kutoa amri ya kiutendaji kwa maslahi ya Qatar na kulinganisha usalama wake na usalama wa kitaifa wa Marekani ni kujaribu kutisha na kuishinikiza Iran isishambulie tena kituo chake cha kijeshi cha al Udaid, kama ilivyofanya mwezi Juni uliopita katika shambulio kali la makombora la kulipiza kisasi, katika kujibu mashambulizi ya anga ya ndege za kivita za Marekani kwenye vituo vyake vya nyuklia. Kwa maneno mengine ni kwamba, serikali ya Marekani itahalalisha jibu la kijeshi la baadaye dhidi ya Iran kwa msingi wa amri ya utendaji ya Trump na kwa kisingizio cha kulinda usalama wa Qatar.