Kisa cha Yasmeen, mkunga katika mji wa Gaza, kinaakisi mateso hayo. “Uchungu ulianza saa 10 alfajiri,lakini hapakuwa na mtu wa kunisaidia,” amesema Yasmeen. “Nilihisi huenda tukafa mimi na mtoto wangu ambaye bado hajazaliwa.”
Mumewe alitoka mbio kwenda kutafuta msaada, lakini hakuweza kupata gari la wagonjwa wala mtu yeyote wa kuwapeleka hospitalini. Yasmeen akalazimika kujifungua nyumbani. “Niliwaomba watoto wangu waweke godoro sakafuni. Sikuwa na dawa zozote za kutuliza maumivu. Sikuwa na budi ila kujifungua mtoto wangu mwenyewe,” amesema
Akiwa anahofia maisha yake na ya mtoto wake, akafanikiwa kujifungua salama, kumkata kitovu mwenyewe, akamvika nguo, na kuanza kumnyonyesha.

Wanawake na wasichana wanatafuta usaidizi katika eneo salama linaloungwa mkono na UNFPA huko Gaza.
Mfumo wa huduma za uzazi waporomoka Gaza
Yasmeen ambaye hapo awali ameweza kuhudumu katika wodi ya wazazi na watoto wachanga katika hospitali ya Al-Shifa,sasa hana tena pa kuhudumia wagonjwa baada ya hospitali hiyo kuharibiwa vibaya kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel. Huduma hizo zimehamishiwa katika hospitali ya wazazi ya Al-Helou, ambako Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi. (UNFPA) hutoa vifaa vya afya ya uzazi, dawa na mahitaji ya akina mama baada ya kujifungua.
Kwa sasa ni vituo 15 pekee vya afya huko Gaza vinavyoweza kutoa huduma za uzazi na watoto wachanga. Vyote vikiwa vimeelemewa kwa wingi wa wagonjwa, upungufu wa vitanda, pamoja na uhaba mkubwa wa dawa na vifaa muhimu. Takribani wanawake 15 hujifungua kila wiki nje ya vituo vya afya bila msaada wa mhudumu mzoefu, jambo linalohatarisha maisha ya mama na mtoto.
Wodi za watoto zaelemewa: Watoto 3 kiatamio kimoja
Dkt. Ahmed, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Mama na Mtoto katika hospitali ya Nasser mjini Gaza, amesema: “Hali ni mbaya sana. Wodi ya dharura ya watoto sasa inapokea idadi ya watoto zaidi ya 1000 kila siku,ambayo ni mara kumi ya idadi ya kawaida.Wakati huohuo, watoto wachanga 200 wamelazwa mahututi, licha ya kuwa na uwezo wa vitanda 40 pekee.”
Dkt. Ahmed ameeleza kuwa hali imekuwa mbaya kiasi kwamba hadi watoto watatu hulazimika kuwekwa kwenye kiatamio kimoja. “Katika saa 24 zilizopita pekee, watoto 13 wamefariki hapa, wakiwemo watoto 10 walifia tumboni na wachanga watatu ambao wamefariki katika viatamio.”
Watoto wazaliwa kabla ya wakati na vifo vinaongezeka
UNFPA imekadiria kuwa kuna takribani wanawake wajawazito 55,000 ambao kwa sasa wamekwama katika mzunguko wa ukimbizi, mashambulizi ya mabomu, njaa kali na utapiamlo, na bila huduma za afya. Kila siku watoto wapatao 130 huzaliwa Gaza, na zaidi ya robo yao huzaliwa kwa njia ya upasuaji. Takribani mtoto mmoja kati ya watano huzaliwa njiti au akiw ana matatizo mengine ya kiafya ikiwemo uzito mdogo.
Vifo vya mama na watoto pia vinaongezeka, huku kuzaliwa njiti na idadi ya watoto kuzaliwa wafu ikiongezeka kutokana na afya duni ya wanawake wanaotaabika na njaa kali, utapiamlo ambao huwafanya kushindwa kubeba mimba hadi mwisho.

Watu wanakimbia kusini kutoka Gaza kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara.
Kukata kitovu kwa kisu kilichopashwa moto
Mkunga Sahar, amesimulia kisa cha rafiki yake aliyeshikwa na uchungu na kujifungua akiwa na ujauzito wa miezi 7 huku akikwama katika kitongoji cha Zeitoun kilichozingirwa mjini Gaza. “Sikuwa na vifaa vyovyote, hata glovu. Nililazimika kutumia kisu nilichokichomeka motoni kukata kitovu na kutumia leso zenye manukato kama bandeji,” ameiambia UNFPA
Sahar pia amekumbuka tukio la mama aliyepoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua. “Hakukuwa na damu ya kumuongezea, hakuna usafiri wa kumhamishia hospitali nyingine, wala daktari wa kumsaidia. Hatukuweza kuzuia damu, akafa na kumuacha mtoto wake mchanga,” amesema kwa majonzi.
Mkunga mwingine, Jenin kutoka Khan Younis, sasa hutoa msaada kwa wanawake wajawazito kutoka kwenye hema dogo aliloweka kwa dharura.

Mkunga kutoka Khan Younis akiwasaidia wanawake wajawazito kutoka kwa hema aliloweka katika eneo la Mawasi.
Huduma za afya Gaza zasalia kwa mashaka
UNFPA imeendelea kuwa msaada, ikianzisha hospitali ya muda ya uzazi huko Nusierat, eneo lililopo katikati mwa Ukanda wa Gaza karibu na mji wa Deir al-Balah, pamoja na kituo cha afya katika eneo la mapokezi la Al-Rashid.
Hata hivyo,mahitaji ni makubwa mno huku usambazaji wa dawa na vifaa ukiwa mdogo. Wadau wa afya wamesema kuwa ikiwa vituo vya afya ambavyo vimesalia Gaza vitalazimika kufungwa, mfumo mzima wa afya utapoteza zaidi ya nusu ya vitanda vyake vya huduma ya mama na mtoto.