Dar es Salaam. Mwanamuziki maarufu wa Bongofleva, Nandy hivi karibuni ameachia wimbo wake mpya, Sweety (2025) akiwa amemshirikisha Jux, huku S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic akiwa amehusika katika utayarishaji wake.
Kolabo hii ambayo imepata mapokezi mazuri ikitazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 1.2 ndani ya siku nne, inaonyesha ni jinsi gani Nandy anafuata nyayo za mume wake Billnass linapokuja suala la wasanii wa kushirikiana nao.
Sweety ni wimbo wenye mahadhi ya Afro Pop unaozungumzia mapenzi kwa njia ya kipekee kwa kuchanganya lugha tatu ambazo ni Kiswahili, Kiingereza na Naija ambayo imeleta neno kama ‘Joro’ katika ngoma hiyo.
Ukiwa umeimbwa kwa sauti laini na mtiririko wa kuvutia masikioni kwa wengi, wimbo huu (Sweety), unabaki kuwa matokeo ya upendo wa dhati na furaha ya kuwa katika hali ya kupenda na hata kupendwa.
Nandy, mwanzilishi wa chapa ya The African Princess, hii ni mara ya kwanza kushirikiana na Jux, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakacha lililotamba na ngoma kama Here We Go (2011) na Facebook Girl (2011).
Jux ambaye ushawishi wake kimuziki umeongezeka hivi karibuni akivutia mashabiki zaidi kutokea Nigeria, hapo awali alikuwa ameshirikishwa na mume wa Nandy, Billnass katika ngoma, Maboss (2024) iliyotayarishwa na S2kizzy.
Maboss ni moja kati ya nyimbo za Billnass zilizopata mapokezi makubwa tena ndani ya muda mfupi. Video (visualiser) yake ambayo imeshutiwa nyumbani kwa Jux, Mbezi Beach, imeshatazamwa YouTube mara milioni 10 ikiwa ni kazi yake ya pili kufanya vizuri katika mtandao huo.
Pengine mafanikio hayo ndio yamefanya Nandy kuona Jux ni msanii sahihi kushirikiana naye wakati huu ambapo ukubwa wa msanii na mafanikio ya kazi zake yanapimwa na namba anazopata katika majukwaa ya kidijitali kama YouTube, Spotify n.k.
Kabla ya kolabo hiyo na Jux, Nandy alikuwa ametoa wimbo wake, Tonge Nyama (2025) ambao alishirikiana na Marioo aliyemwandikia ngoma ‘Wasikudanganye’ iliyojumuishwa katika albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018).
Ukiwa umetayarishwa na S2kizzy pia, Tonge Nyama ni wimbo uliochukua msemo wa mtaani na kuutumia kuelezea hali ya mtu kuvutiwa sana na mwingine hadi kufikia hatua ya kutamani kuwa naye karibu kimwili na kihisia.
Kazi hiyo imethibitisha umahiri wa Nandy si tu katika uimbaji, bali pia katika kuwasilisha ujumbe mzito kwa njia rahisi ya kiburudani kwa kuzingatia matumizi sahihi ya lugha ya kisanaa.
Hata hivyo, licha ya maandalizi mazuri na matarajio makubwa, wimbo ‘Tonge Nyama’ haujafika pale ulipotegemewa kufuatia kukumbwa na kesi ya hakimiliki iliyopelekea hadi kuondolewa YouTube, kisha Nandy kushtakiwa mahakamani.
Nandy kushirikiana na Marioo ilikuwa ni mwendelezo tu wa kufuata nyayo za Billnass ambaye hapo awali alishatoa kolabo mbili na mkali huyo wa Bad Nation ambazo ni Deka (2020) na Maokoto (2023), zote zikitayarishwa na S2kizzy.
Wimbo ‘Maokoto’ ulifanya vizuri hadi kuwania Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 kama Video Bora ya Mwaka ikishindana na kazi nyingine kama Sele (Mbosso), Nani Remix (Zuchu), Single Again Remix (Harmonize) na Achii (Diamond) iliyoshinda.
Kwa muktadha huo, tutarajie Nandy kuja kushirikiana na wasanii wengine waliowahi kufanya kazi na mumewe na zikabamba. Miongoni mwa tunaoweza kuwategemea, ni Jay Melody aliyeshiriki katika ngoma ya Billnass, Puuh (2022) iliyoshinda TMA.
Ikumbukwe Nandy, mshindi wa TMA mara tano, alianza safari ya muziki mwaka 2010 aliporekodi kwa mara ya kwanza, na baadaye alijiunga na B Band ambapo alitumbuiza pamoja na Banana Zorro kwa kipindi cha miaka kadhaa.
Mafanikio yake yalianza kuonekana baada ya kushiriki shindano la Tecno Own the Stage 2015/16 lilofanyika Nigeria na kushika nafasi ya pili. Baadaye, msanii huyo mwenye kipaji kikubwa alijiunga na lebo ya Epic Records Tanzania.
Alivuma zaidi alipotoa kibao chake, Nagusagusa (2016) baada ya kunolewa na Tanzania House of Talent (THT) ambayo imewatoa wanamuziki kama Mwasiti, Barnaba, Linah, Amin, Ruby, Ibrah Nation, Recho Kizunguzungu, Jolie, Ally Nipishe n.k