Utafiti wa kitaaluma umefichua jinsi kampeni ya kisasa inayotumia Akili Mnemba(AI) ilivyolenga kuchochea harakati za uasi ndani ya Iran, wakati wa vita vya kichokozi na vilivyokuwa kinyume cha sheria vilivyoendeshwa na utawala wa Israel na Marekani dhidi ya taifa la Iran mnamo mwezi Juni.

Matokeo ya utafiti huo, uliofanywa na Chuo Kikuu cha Clemson huko South Carolina nchini Marekani yalichapishwa Alhamisi na kituo cha utafiti cha Citizen Lab, kilicho ndani ya Shule ya Munk ya Masuala ya Kimataifa na Sera ya Umma, katika Chuo Kikuu cha Toronto.

Kampeni hiyo, iliyoanzishwa mwaka 2003, ilitambuliwa kama njama ya nje iliyopangwa kwa ustadi, huku utawala wa Israel ukitajwa kama mshukiwa mkuu kwa ushirikiano wa Marekani.

Mtandao huo ulioratibiwa kwa kiwango cha juu ulihusisha zaidi ya akaunti bandia 50 kwenye X (zamani Twitter), zilizoundwa kwa kutumia AI ili kuwachochea Wairani kuchukua hatua za uasi dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa nchi yao.

Kampeni hiyo ilizidi kushika kasi baada ya Januari, na kufikia kilele wakati wa vita vya Juni 13–25 vilivyopelekea Wairani wasiopungua 925 kupoteza maisha, na kulenga miundombinu ya nyuklia, kijeshi na kiraia ya Jamhuri ya Kiislamu.

Lengo lilikuwa kuchochea machafuko mara tu baada ya mashambulizi ya Israel, ikiwemo lile lililolenga gereza la Evin jijini Tehran, ambapo watu wasiopungua 80 walipoteza maisha.

Uchambuzi ulionyesha kuwa mtandao huo huenda uliendeshwa na shirika la utawala wa Israel au wakandarasi waliodhibitiwa kwa karibu, wakitumia teknolojia ya AI kutengeneza video, picha na simulizi za vurugu na machafuko.

Akaunti hizo bandia zilichapisha video zilizotengenezwa na AI na kujitahidi kuonekana halisi kwa kutaja vyombo vya habari vinavyopinga Iran.

Machapisho yaliyopangwa yalihamasisha raia “kuwaachilia wafungwa” baada ya shambulizi la gereza la Evin, huku yakitoa taarifa za uongo kwamba eneo hilo lilikuwa salama.

Watafiti walitaja kampeni hiyo kama operesheni nadra ya “ushawishi wa moja kwa moja,” ikitumia udanganyifu wa AI kusukuma ajenda ya uasi.

Mnamo Juni 15, machapisho ya kughushi yalidai kuwa uchumi wa Iran umeporomoka na kuna ufisadi mkubwa, yakihamasisha raia kuondoa fedha zao kwenye benki. Aidha kampeni hiyo ilipandikiza chuki dhidi ya uongozi wa Kiislamu nchini Iran.

Kuanzia Juni 20 hadi 22, mtandao huo ulichochea maandamano ya usiku kupitia hashtagi #8OClockCry, ukihamasisha waandamanaji kutoa kauli za kupinga Iran.

Video za deepfake na picha zilizorudiwa zilihaririwa kuonyesha maandamano, kauli za uasi na machafuko, jambo lililoonyesha kiwango cha kitaalamu na uratibu wa hali ya juu wa kampeni hiyo.

Hata hivyo, wachambuzi waliotoa maoni kuhusu utafiti huo walisema kampeni hiyo ilishindwa vibaya, kwani taifa la Iran lilijikusanya kwa nguvu nyuma ya uongozi na majeshi yake katika kipindi hicho cha siku 12, huku likidumisha mshikamano wa kitaifa.

Hii si mara ya kwanza kwa utawala wa Israel kutajwa kuhusika na kampeni za uasi dhidi ya taifa la Iran.

Katika kipindi chote cha vita, utawala huo ulitegemea mtandao wa majasusi na vibaraka waliolenga kusaidia kusukuma ajenda zake za kupinga Iran na kuvuruga umoja wa kitaifa.

Vibaraka na majasusi hao walikabiliwa vikali na Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran, ambayo ilisaidia kuwakamata watu kadhaa waliokuwa wakihudumu kwa niaba ya Tel Aviv.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *