Viongozi wa kimataifa wamekaribisha hatua ya awali ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, ya kukubali kushiriki katika mazungumzo ya amani yaliyosubiriwa kwa muda mrefu, yakilenga kumaliza vita vya miaka miwili vya mauaji ya kimbarii vinavyoendeshwa na Israel dhidi ya Gaza.

Hatua hii imekuja baada ya Hamas kuwasilisha Ijumaa jibu lake kwa pendekezo la vipengele 20 lililotumwa na Rais wa Marekani Donald Trump, likidai kuhitimisha hujuma ya  Israel dhidi ya Gaza.

Harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestine, yenye makao yake Gaza imesema inakubali “kuwaachilia mateka wote Waisraeli, walio hai na waliopoteza maisha.” Aidha Hamas imeidhinisha “kukabidhi usimamizi wa Ukanda wa Gaza kwa chombo huru cha Wapalestina (wataalamu wa kiufundi) kwa msingi wa makubaliano ya kitaifa ya Wapalestina na kwa msaada wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.”

Hamas imeeleza kuwa jibu lake limetokana na “wajibu wa kitaifa na kwa kuzingatia misingi, haki na maslahi ya juu ya watu wetu.”

Trump amesema jibu la Hamas linaonesha kuwa kundi hilo la Muqawama “liko tayari kwa amani ya kudumu,” na akaitaka Israel “kusitisha mara moja mashambulizi ya anga dhidi ya Gaza.”

Katika ujumbe wa video, Rais wa Marekani ameahidi kuwa pande zote zitashughulikiwa kwa haki katika mazungumzo ya Gaza, akitaja hatua ya Hamas ya kukubali kuwaachilia mateka kama “siku ya kipekee.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza tamko la Hamas, ambapo msemaji wake Stephane Dujarric amesema kiongozi huyo wa UN “anazitaka pande zote kutumia fursa hii kumaliza mgogoro wa kusikitisha huko Gaza.”

Viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Australia, Italia na Uturuki pia wamekaribisha hatua ya Hamas ya kukubali mpango huo wa amani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majed al Ansari, amesema Doha “inakaribisha tangazo la Hamas la kuidhinisha kwa misingi ya awali pendekezo la Rais Trump,” na amethibitisha kuwa kuna uratibu unaoendelea na Misri pamoja na Washington wa kuendeleza upatanishi.  

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeeleza kuwa jibu la Hamas ni “hatua chanya” inayoakisi “nia ya makundi yote ya Wapalestina ya kuepusha umwagaji damu ya watu wa Palestina.” Qatar na Misri ni wapatanishi wakuu kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni.

Rais Gustavo Petro wa Colombia, amesema anakubaliana na Trump “kwa mara hii,” huku akitaka “kusitishwa kwa mauaji ya kimbari.”

Petro ameongeza kuwa endapo Trump “atahamasisha jeshi lake kusitisha ukandamizaji dhidi ya Palestina, basi jeshi hilo litaandamana na jeshi la Colombia.”

Mpango wa Trump umetolewa huku Marekani ikiendelea kutoa msaada wa kijeshi, kijasusi na kisiasa kwa Israel, msaada ambao umechochea mauaji ya kimbari ya Wapalestina zaidi ya 66,000—wengi wao wakiwa wanawake na watoto—katika Ukanda wa Gaza tokea Oktoba 2023.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *