
Katika mahojiano maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa ya Kifaransa kufuatia taarifa yake ya karibuni kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Bi. Keita, ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa kulinda amani wa UN, nchini DRC, MONUSCO, ametoa mtazamo kuhusu shughuli za sasa za ujumbe huo, changamoto zilizopo mashinani, na ujumbe wa matumaini kwa wananchi wa Kongo.
Machafuko Ituri: Kuongezeka kwa kuhamahama kutokana na ghasia
Akisisitiza hali mbaya ya usalama huko jimboni Ituri, mashariki mwa DRC, Bi. Keita ametaja mashambulizi yanayoendelea kutoka makundi mbalimbali ya waasi, hasa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) — kundi linalojulikana kwa mauaji ya raia kwa kiwango kikubwa.
“ADF ni kundi linalosafiri kwa haraka na lina wepesi wa kujipanga. Kukabiliana na hili, MONUSCO imebadilisha mkakati wake wa operesheni,” amesema.
Badala ya kutegemea tu kambi za kijeshi zilizowekwa, MONUSCO sasa imeanzisha kambi zinazohama na doria za haraka kwa kushirikiana na jeshi la serikali ya DRC, (FARDC), hali ambayo imeboresha uwezo wao wa kuitikia vitisho na kulinda raia.
“Ushirikiano na mamlaka ya jimbo la Ituri umekuwa mzuri,” Keita amebainisha, akieleza kuhusu ushirikiano ulioboreshwa na serikali za mitaa na wadau wa kanda, wakiwemo jeshi la Uganda (UPDF).
Amesisitiza kuwa mkakati huu wa pamoja ni muhimu sana katika kukabiliana na hali tata ya Ituri, ambako makundi ya wanamgambo ya kikabila kama CODECO na Zaire yanaendelea kufanya mashambulizi ya kisasi dhidi ya jamii za wenyeji.
Kusaidia ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa amani
Bi. Keita pia ameeleza kuhusu msaada wa MONUSCO kwa ushiriki wa maana wa wanawake katika mchakato wa amani. Kupitia mafunzo kwa wanawake wapatanishi wa ndani na mabalozi wa amani, ujumbe huo unasaidia kupaza sauti za wanawake katika ngazi zote — kuanzia za mitaa hadi kitaifa.
“Wanawake wa DRC hawangoji waalikwe mezani,” amesisitiza. “Wanatoa mapendekezo yao, wanatetea ushirikishwaji, na wanajipenyeza kwenye mchakato — hata kabla ya kupewa nafasi rasmi.”
Ujumbe kwa wananchi wa DRC: Subira na matumaini
Katika hitimisho lake, Bi. Keita ametuma ujumbe moja kwa moja kwa wananchi wa DRC.
“Kwanza kabisa, nataka kueleza huruma na mshikamano mkubwa. Uvumilivu wa watu wa DRC mbele ya matatizo yanayoendelea ni wa kuigwa. Najua mchakato huu unaonekana mrefu na wenye uchungu, lakini naomba subira iendelee. MONUSCO, serikali ya DRC, Umoja wa Afrika, na jamii ya kimataifa wote wamejitolea kwa dhati kuleta amani ya kudumu mashariki mwa DRC.”