Mamilioni ya watu nchini Somalia wanakabiliwa na njaa inayozidi kuwa mbaya, kufuatia kupunguzwa kwa misaada ya wafadhili, hali inayoliweka shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) katika upungufu mkubwa wa ufadhili.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, taifa hilo la Pembe ya Afrika ni miongoni mwa maeneo yaliyo hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi, na katika kipindi cha miaka mitano iliyopita limekumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo minne, pamoja na mafuriko ya kihistoria yanayofanana na yale ya karne moja iliyopia.

Mnamo Novemba, watu wapatao 750,000,  zaidi ya theluthi mbili ya walengwa wa sasa,  wanatarajiwa kuondolewa kwenye mpango wa dharura wa chakula wa WFP.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa shirika hilo, inaweza “kuwasukuma walioathirika zaidi katika hali ya janga la kibinadamu.”

Ross Smith, Mkurugenzi wa WFP wa maandalizi ya dharura akizungumza akiwa mjini Nairobi amesema: “Tunaona ongezeko hatari la viwango vya dharura vya njaa, huku uwezo wetu wa kutoa msaada ukizidi kupungua kila siku.”

WFP inaongoza operesheni kubwa zaidi ya kibinadamu nchini Somalia, na inachangia zaidi ya asilimia 90 ya mwitikio wa usalama wa chakula nchini humo.

“Kiwango cha sasa cha msaada kiko chini sana ikilinganishwa na mahitaji yanayoongezeka,” Smith ameongeza.

Takwimu za serikali zilizotolewa mwezi Agosti zinaonyesha kuwa watu milioni 4.4 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula katika taifa hilo linalokumbwa na migogoro.

Takriban watoto milioni 1.7 walio chini ya umri wa miaka mitano tayari wanakabiliwa na utapiamlo mkali — wakiwemo 466,000 walioko katika hali ya hatari — lakini WFP imesema ni watoto 180,000 pekee wanaopokea matibabu ya lishe kwa sasa, idadi ambayo huenda ikapungua zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *