
FAUSTIN akasema kwenye simu: “Hello, mama…!” Sauti yake hakuonyesha huzuni hata chembe.
“Ndiyo, mwanangu — uko wapi?”
“Niko polisi.”
“Umekamatwa kwa kosa gani?”
“Sijakamatwa. Nimejileta mwenyewe.”
“Umefanya nini?”
“Kama alivyokueleza afisa wa polisi hapa, nimewaua watu waliomuua ndugu yangu Thomas. Walihukumiwa kunyongwa lakini wakatoroshwa jela, ili kuupinda mkondo wa sheria. Sikukubaliana na hilo.”
“Ni kweli ulifanya hilo kosa, Faustin?”
“Nimelifanya ndiyo, lakini hilo sio kosa, mama, kwa sababu wale watu walishahukumiwa kunyongwa. Mimi nilitekeleza hukumu ya mahakama.”
“Kama sio kosa, mbona umekamatwa”
“Sijakamatwa. Nimejileta mwenyewe polisi kuwapunguzia kazi ya kumtafuta mtu aliyewaua wafungwa wale.”
“We, mwanangu, ni mzima kweli?”
“Ni mzima, mama. Suala la kuuawa kwa Thomas limeniuma sana.”
“Lakini baada ya kuwaona hao watu wametoroshwa, ungekwenda kuwaripoti polisi?”
“Kazi ya polisi ni kukamata wahalifu na kuwashitaki; wale watu walishakamatwa, walishashitakiwa na pia walishahukumiwa. Sasa, ulitaka niwaripoti polisi kwa ajili gani? Wale walitakiwa kuuawa tu kama mahakama ilivyowaamulia!”
“Mwanangu, umeshajitia kwenye matatizo na serikali. Unadhani watakuachia”
“Najua hawataniachia, lakini sijutii kitendo changu.”
“Wewe hujutii kitendo chako, lakini utanipa mimi usumbufu usio na sababu ya msingi.”
“Njoo tu, mama yangu, ili ujue nitakachokutana nacho mwanao.”
“Hebu mpe simu huyo polisi.”
Faustin akanipa simu.
“Hello, mama wa Faustin…!” nikasema.
“Ndiyo kaka, sasa itakuwaje?”
“Uchunguzi wetu ukikamilika tutamfikisha mahakamani mwanao. Mahakama ndio yenye uamuzi.”
“Sasa, mimi ninakuja huko?”
“Utakuja lini?”
“Kesho au keshokutwa.”
“Ninaakutakia safari njema, lakini utakapofika njoo kituo kikuu cha polisi uulize Inspekta Fadhil.”
“Sawa. Nitafika.”
“Sawa.”
Nikakata simu na kumtazama afisa upelelezi aliyekuwa akinitazama mimi.
“Umemsikia, mama yake. Alikuwa hajui chochote. Amesema atakuja keshokutwa.”
“Tunamsubiri.”
Nikamatazama Faustin.
“Sasa Faustin, nakwenda kukuweka ndani ili niweze kukufungulia faili,” nikamwambia.
Nilipomwambia hivyo, Faustin hakunijibu kitu. Pengine alikuwa ameshaanza kufadhaika baada ya kugundua kuwa tutamfikisha mahakamani.
Huenda alipojileta mwenyewe polisi alikuwa na imani kwamba polisi tungemuachia kwa vile watu aliowaua walishaamuliwa na mahakama wafe kwa kunyongwa.
Kwa mtu asiyejua sheria za nchi anaweza kudhani hivyo.
Wako watu waliowaua wezi baada ya kuwakamata kwa kudhani kuwa kwa vile ni wezi hata ukiwaua hutakuwa na hatia. Matokeo yake, wengi waliothibitika kufanya hivyo walipata adhabu za vifungo au kunyongwa kwa kuua kwa kukusudia.
Huenda hivyo ndivyo alivyowaza Faustin mpaka akaamua kujileta mwenyewe polisi.
Baada ya kumuweka ndani, Faustin nilishirikiana na afisa upelelezi kumfungulia faili lake — ambapo tungetia malezo ya Faustin mwenyewe, maelezo ya mama yake na maelezo mengine yaliyohusu uchunguzi wetu.
Niliporudi nyumbani jioni nilijitupa kwenye sofa kisha nikashusha pumzi ndefu za faraja.
Nilikuwa kama niliyeutua mzigo mzito kutoka kichwani mwangu. Kujitokeza kwa Faustin na kukiri yeye mwenyewe kwamba ndiye muuaji tuliyekuwa tunamtafuta, ilikuwa kama niliyetua mzigo mzito uliokuwa ukinilemea.
Ile faraja iliyokuwa ndani ya moyo wangu ilinifanya nimpigie simu Hamisa.
Nilikuta simu ya Hamisa inatumika; moyo wangu ukashituka.
“Anaongea na nani?” nikajiuliza.
Iliwezekana alikuwa anazungumza na mtu yeyote — ndugu, rafiki au mtu mwingine — lakini kwa vile sikuwa na uhakika nilianza kuhisi wivu.
Nilikata simu huku nikijisikia kufadhaika.
Baada ya muda kidogo nikapiga tena. Bado simu ilikuwa ikitumika.
Sasa moyo ulianza kuniuma.
Kweli, upendo ni upumbavu, nikajiambia. Hamisa anaweza kuwa anazungumza na ndugu yake au rafiki yake au mtu yeyote anayemheshimu, nikajieleza.
Lakini moyo wangu uliendelea kuniuma. Moyo huo uliniambia kuwa Hamisa anaweza kuwa anaongea na mwanaume wake.
Wazo hilo likanifanya nimpigie tena bila kusubiri zaidi. Lakini simu yake ilikuwa bado ikitumika.
Inawezekana anaongea na mwanaume, nikajiambia kwa uchungu. Nikakata simu.
“Lazima atakuwa na mwanaume mwingine,” nikajiambia kwa uchungu. “Wanawake hawaaminiki.”
Wakati nikiwa nawaza hivyo, simu ikaita. Nilipotazama skrini nikaliona jina la Hamisa.
Nikaipokea simu haraka.
“Hello… Hamisa… mbona unaniumiza moyo wangu?” nilimuuliza.
“Kwanini?” akaniuliza.
“Unazungumza na nani muda wote huo?”
Hamisa akacheka. Alitoa kicheko kidogo lakini cha kusisimua.
“Unadhani nilikuwa naongea na wanaume?” akaniuliza.
“Ndiyo maana yake.”
“Acha wivu wako! Nilikuwa naongea na mama.”
“Oh! Kumbe ulikuwa unaongea na mama mkwe! Hajambo?”
“Hajambo. Nilikuwa nazungumza naye kuhusu ile habari…”
“Habari ipi?”
“Ya kurudisha uchumba wetu.”
Hamisa aliponiambia hivyo nilihisi kama aliyeumwagia maji baridi moyo wangu uliokuwa moto.
“Lakini ulimueleza vizuri?”
“Ndiyo, nilimueleza vizuri.”
“Kwamba uchumba wetu umerudi kama zamani?”
“Ndiyo.”
“Amesemaje?”
“Amefurahi. Wao hawana kauli, wananisikiliza mimi tu.”
“Unakumbuka nilikwambia nataka tuoane haraka”
“Unadhani harusi ni kitu cha mara moja tu? Ni lazima watu wajiandae.”
“Ndiyo, lakini sipendi ifike miezi mitatu.”
“Kwani tutaoana wapi?”
“Hapa hapa jijini.”
“Itabidi wazazi na ndugu tuwaite huku.”
“Ndiyo.”
“Ni sawa, lakini si unajua kuna vikao vya ndugu na marafiki? Hatuwezi kukurupuka.”
“Ninajua.”
“Kama unajua, acha pupa. Acha twende kwa utaratibu.”
“Hii chelewa-chelewa ndio inayosababisha mikwaruzano.”
“Hakutakuwa na mikwaruzano. Unajua wewe ndiye mkorofi lakini mimi sina tatizo.”
“Hakuna haja ya kubishana. Nataka tuende vizuri. Wasiliana na wazazi wako ili muhakikishe hili suala halitachukua muda. Nataka nikuweke ndani.”
“Ndani — polisi au…?”
Nilicheka nikamwambia Hamisa:
“Nikuweke ndani nyumbani.”
“Usijali, utaniniweka.”
“Sawa. Suala jingine nililotaka kukufahamisha ni kuhusu yule muuaji niliyekuwa nikimtafuta.”
“Ana nini?”
“Amejitokeza mwenyewe leo. Kwa kweli nimefurahi. Nimehisi kama nimetua mzigo mzito uliokuwa ukinilemea.”
“Ah! Amejitokea mwenyewe?”
“Yaani, ametusumbua sana. Kumbe ni ndugu yake Thomas, yule kijana aliyeuawa, na alikuwa anaua kulipa kisasi kwa sababu wale waliomuua ndugu yake walikuwa bado wako hai baada ya kutoroshwa jela.”
“Lakini amefanya vizuri, amewasaidia kazi.”
“Alichofanya ni kinyume cha sheria. Hatuwezi kumpongeza. Tutamfikisha mahakamani.”
Nikamsikia Hamisa akiguna.
“Sawa. Naenda kupika. Kama utaweza utanipigia usiku.”
“Poa.”
Hamisa akakata simu.
Hazikupita hata sekunde thelathini afisa upelelezi akanipigia simu. Nilipoona jina lake nikaipokea simu haraka.
“Ndiyo, afande…”
“Kuna kitu tulisahau kukizungumza,” afisa upelelezi akanieleza kwenye simu.
“Kitu gani, afande?”
“Kwamba kesho asubuhi uchukue askari mwende mkapekue chumba cha yule kijana huko Pongwe na pia muijue nyumba aliyokuwa akiishi.”
“Ni sawa. Tutafanya hivyo asubuhi.”
“Jambo jingine ni kwamba chukua alama zake za vidole; tutafute kama ana rikodi za uhalifu katika kumbukumbu zetu.”
“Sawa, afande.”
“Vijana wa aina yake ni hatari. Mtu huwezi kufanya uhalifu mkubwa kabla ya kuanza na uhalifu mdogo mdogo.”
“Ni kweli, afande.”
“Hiyo shughuli utaifanya kesho.”
“Sawa, afande.”
“Kingine ni kuhusu wale watu aliowanyonga. Miili yao bado haijachukuliwa hospitali. Nimeombwa nitoe kibali ili wazikwe na jiji. Unadhani hatutaihitaji tena ile miili?”
“Tusubiri hadi hapo kesho tutakapokutana.”
“Sawa.”
Afisa upelelezi akakata simu.
Asubuhi ya siku iliyofuata nilipofika kituoni, niliagiza Faustin aletwe ofisini kwangu.
Polisi mmoja aliyekwenda kumtoa mahabusi alimleta ofisini kwangu.
“Tunataka utupeleke nyumbani kwako,” nikamwambia.
“Mimi naishi Pongwe,” akajibu.
“Twende huko, Pongwe.”
“Sawa.”
Nilichukua polisi wanne, wawili wakiwa na bunduki, tukaondoka na kijana huyo kuelekea kitongoji cha Pongwe, ambacho kipo takriban kilomita kumi na tano kutoka jijini Tanga.
Tulipofika Pongwe Faustin alituonesha mtaa aliokuwa akiishi. Nyumba aliyopanga chumba lilikuwa banda tu la uani lililokuwa na vyumba vinne, jiko pamoja na choo.
“Unaishi hapa” nikamuuliza alipotuonyesha nyumba hiyo.
“Ndiyo, ninaishi hapa.”