
Michuano ya Kombe la Dunia 2026 inatarajiwa kuwa ya kihistoria si tu kwa ukubwa wake, bali timu zinazokwenda kushiriki kwani hii ni mara ya kwanza, mataifa 48 yatashiriki fainali hizo zitakazochezwa katika nchi tatu za Marekani, Canada na Mexico, kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, 2026. Tayari maandalizi yanaendelea, huku Afrika ikisaka wawakilishi wake tisa wanaofuzu moja kwa moja.
Awali ilikuwa timu tano za Afrika ndizo zinashiriki Kombe la Dunia, lakini baada ya timu shiriki kuongezwa, imepatikana fursa hiyo ya kupeleka timu tisa zinazofuzu moja kwa moja, lakini kuna uwezekano zikawa kumi kwani nyingine inapitia hatua ya mtoano ya mabara (Inter-Confederation Play-offs). Hadi sasa, michuano ya kufuzu imekuwa na ushindani mkali, kuna timu zilipewa nafasi kubwa ya kufuzu, lakini hadi sasa mambo yamekuwa magumu.
Morocco na Tunisia zapenya mapema
Kati ya mataifa 54 yaliyoshiriki hatua ya makundi kufuzu Kombe la Dunia 2026 kutokea Afrika, Morocco na Tunisia ndizo pekee hadi sasa zimejihakikishia nafasi zao za kwenda kushiriki mashindano hayo. Morocco, ambayo ipo Kundi E sambamba na Tanzania, Niger, Zambia, na Congo, imekusanya pointi 21 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine zikiwa zimebaki mechi mbili.
Morocco imefuzu kwa mara ya saba katika historia baada yam waka 1970, 1986, 1994, 1998, 2018 na 2022. Mafanikio yao yanaonyesha uimara wa mfumo wa soka wa taifa hilo, hasa baada ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika hatua ya nusu fainali.
Tunisia nayo imefuata nyayo, ikiibuka kinara wa Kundi H. Taifa hilo litakuwa linakwenda kushiriki kwa mara ya saba baada ya mwaka 1978, 1998, 2002, 2006, 2018 na 2022. Kwa mafanikio haya, Morocco na Tunisia zimethibitisha kuwa nguvu ya kaskazini mwa Afrika bado inatamba.
Vita ipo hapa
Huku mataifa hayo mawili yakijihakikishia tiketi mapema, vita ya kufuzu imebakia mikononi mwa mataifa mengine saba yatakayoungana nao moja kwa moja. Kundi C na F ndiyo kuna msisimko zaidi kutokana na ushindani wa karibu kati ya timu za juu.
Awali Afrika Kusini ilikuwa kinara wa kundi C kwa pointi 17. Hata hivyo, adhabu kutoka FIFA kwa kumchezesha mchezaji mwenye kadi imerudisha nyuma matumaini yao, pointi zikapunguzwa hadi kufikia 14.
Sasa Benin ndio inaongoza, ikiwa na pointi sawa (14), lakini zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa. Chini yao, Nigeria na Rwanda zinapambana zikiwa na pointi 11 kila moja.
Iwapo Nigeria na Rwanda zitashinda mechi zao mbili za mwisho, zitafikisha pointi 17, na kuibua mabadiliko makubwa kwenye kundi. Hii inamaanisha hatma ya kundi hili itaamuliwa dakika za mwisho kabisa.
Ukija Kundi F, Ivory Coast, mabingwa wa Afrika 2023, wanaongoza kwa pointi 20, wakifuatiwa kwa karibu na Gabon wenye 19.
Ivory Coast inakabiliwa na Seychelles ugenini na Kenya nyumbani, mechi ambazo kwa wastani zinaonekana rahisi, lakini presha ya kutaka kufuzu inaweza kubadilisha mambo. Gabon, kwa upande mwingine, inaanza ugenini dhidi ya Gambia kabla ya kumalizia nyumbani dhidi ya Burundi.
Iwapo Gabon itashinda michezo yote miwili, inaweza kufikisha pointi 25 na kuwazidi Tembo wa Ivory Coast ikiwa hawawezi kushinda mechi zote.
Zipo karibu kufuzu
Mbali na makundi hayo yenye ushindani, mataifa kama Misri, Senegal, Algeria, Ghana na Cape Verde yako hatua moja tu kufuzu moja kwa moja. Timu hizi zinahitaji ushindi wa mechi moja kati ya mbili zilizobaki.
Kwa upande wa historia ya ushiriki, Algeria imeshiriki mara nne (1982, 1986, 2010 na 2014) sawa na Ghana (2006, 2010, 2014 na 2022). Misri imeshiriki mara tatu (1934, 1990 na 2018) kama Senegal (2002, 2018 na 2022), huku Cape Verde, kwa upande wake, inaweza kuandika historia ya kipekee iwapo itafuzu kwa mara ya kwanza kabisa.
Namna ya kufuzu kupitia mtoano
Kwa timu ambazo hazitamaliza nafasi ya kwanza kwenye makundi yao, bado kuna fursa nyingine. Timu nne bora kati ya zilizomaliza nafasi ya pili zitapewa nafasi ya kucheza hatua ya mtoano wa CAF.
Mtoano huo utazipambanisha timu hizo nne, na mshindi wa jumla atawakilisha Afrika kwenye Inter-Confederation Play-offs, hatua ambayo itawakutanisha na mataifa kutoka mabara mengine kwa tiketi ya mwisho ya Kombe la Dunia.
Kwa sasa, miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa ya kuingia kwenye mtoano ni Gabon yenye pointi 19, Madagascar (16), DR Congo (16), Burkina Faso (15), Cameroon (15), Namibia (15), Uganda (15), Afrika Kusini (14) na Tanzania (10).
Mtoano wa mabara (Inter-Confederation Play-offs)
Mshindi wa mtoano wa Afrika ataungana na wawakilishi kutoka mabara mengine katika hatua maalum ya mtoano wa mabara.
Hadi sasa, tayari zipo timu mbili zilizojihakikishia kucheza hatua hiyo ambazo ni New Caledonia kutoka Oceania (OFC) na Bolivia kutoka CONMEBOL (Amerika Kusini). Mabara yanayosubiria nafasi hiyo ni mwakilishi mmoja kutoka Asia (AFC), wawakilishi mmoja kutoka CONCACAF (Amerika Kaskazini na Kati) na mwakilishi mmoja kutoka Afrika (CAF).
Hatua hii itakuwa na ushindani mkubwa, kwani itatoa nafasi moja pekee kwa timu kushiriki Kombe la Dunia, ikimaanisha kila mchezo utakuwa kama fainali.
Safari ya Tanzania
Tanzania ambayo ipo Kundi E, imekuwa na safari ngumu ya kufuzu. Kutokana na Morocco kujihakikishia nafasi ya kwanza, Taifa Stars haina tena nafasi ya kufuzu moja kwa moja. Hata hivyo, inaendelea kupigania nafasi ya heshima ya kumaliza juu zaidi.
Kwa pointi 10 ilizonazo, Tanzania ina nafasi ndogo sana ya kuingia kwenye orodha ya timu nne bora za nafasi ya pili.
Oktoba 8, mwaka huu, Tanzania itakuwa mwenyeji wa Zambia katika mechi ya mwisho ya kufuzu. Kundi hili lina upungufu wa mechi kufuatia Eritrea kujitoa, hivyo zimebaki timu tano, kila moja inashuka dimbani mara nane na sio kumi kama makundi mengine yenye timu sita.
Mfumo mpya wa mashindano
Kombe la Dunia 2026 itakuwa na sura mpya kabisa. Badala ya timu 32 kama ilivyokuwa kawaida, sasa zitakuwa 48, zikiwa zimegawanywa katika makundi 12 ya timu nne kila moja. Timu mbili za juu na nane bora zitakazomaliza nafasi ya tatu zitasonga mbele hatua ya mtoano wa 32 bora.