
Na hivi karibuni, Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Deco alisema kuwa Rashford anawapa kile ambacho walikitegemea.
Barcelona, Hispania. Marcus Rashford ameweka lengo la kupiga pasi za mwisho 30 hadi 40 katika msimu huu akiwa na kikosi cha Barcelona.
Nyota huyo wa England anacheza Barcelona kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kununuliwa kwa Pauni 26 milioni mwishoni mwa msimu.
Mwanzo mzuri ambao amekuwa nao katika kikosi cha Barcelona msimu huu unaonekana kumshawishi Rashford kuweka lengo ambalo halionekani kama anaweza kulitimiza kwa urahisi.
Katika mechi tisa ambazo ameshacheza msimu huu akiwa na Barcelona katika mashindano tofauti, Rashford tayari ameshafunga mabao mawili na kupiga pasi tano za mwisho.
Miongoni mwa mabao hayo mawili, moja amefunga katika mchezo wa ugenini wa Barcelona dhidi ya Newcastle United ambao timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika Uwanja wa St James Park.
Kama akitimiza hilo, Rashford atapiku kile alichokifanya katika misimu mitatu iliyopita ambapo ambapo kiujumla alipiga pasi za mwisho 27.
Na kuanza vizuri ndani ya Barcelona msimu huu kumekuwa na faida kwa Rashford kwani juzi aliteuliwa kuwemo katika kikosi cha wachezaji 24 wa England kinachojiandaa na mechi mbili za kimataifa mwezi huu.
Oktoba 9 mwaka huu, England itacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki na Wales na siku tano baadaye itacheza na Latvia katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia.
Rashford amejumuishwa kundini huku baadhi ya mastaa wakiachwa mfano akiwa ni Jude Bellingham wa Real Madrid ambaye ameachwa kwa kile kilichotajwa na Tuchel kuwa hajafikia ubora wake.
Kuanza vizuri kwa Rashford katika kikosi cha Barcelona kunamuweka katika matumaini ya kuwemo katika kikosi cha England kwenye Fainali zijazo za Kombe la Dunia ambazo zitafanyika Marekani, Canada na Mexico mwakani.
Na hivi karibuni, Mkurugenzi wa Michezo wa Barcelona, Deco alisema kuwa Rashford anawapa kile ambacho walikitegemea.
“Ni mapema mno kuzungumzia uamuzi wa dirisha lijalo la majira ya kiangazi lakini cha msingi ni kwamba tuna furaha na yeye. Ambacho tulifikiria atatuletea, anatuletea, alisema Deco.