
Ving’ora vya mashambulizi ya anga vimesikika katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) kufuatia kombora la balestiki lililovurumishwa na Jeshi la Yemen ili kulipiza kisasi vita vya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Gaza.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, shambulio hilo jipya la kombora kutoka Yemen limepelekea kusikika ving’ora katika baadhi ya maeneo ya Israel pamoja na kusini mwa Ukingo wa Magharibi, mapema leo Jumapili.
Tovuti ya habari ya Ynet imeripoti kuwa sauti za ving’ora zimesikika katika maeneo ya Be’er Ya’akov, Lod, Rehovot, na Modi’in katika eneo la Shefela, na pia katika makazi ya Lakishi na katika Ukingo wa Magharibi.
Vyombo vya habari vya Israel pia vimethibitisha kuwa anga ya Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion imefungwa kwa muda kufuatia kombora hilo la Yemen .
Shambulio la kombora la jeshi la Yemen limeibua taharuki kubwa miongoni mwa walowezi haramu wa Kizayuni na hivyo kupelekea maelfu ya Wazayuni kuyaacha makazi yao.
Vikosi vya Yemen vimetekeleza mzingiro wa kimkakati wa baharini wenye lengo la kuvuruga na kuzuia utumaji silaha kwa Israel zinazotumika katika mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.