Katika hatua iliyoratibiwa, viongozi wa nchi kubwa za Ulaya wamekaribisha jibu la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (HAMAS) kwa mpango wa Trump kuhusu Gaza.

Wakuu wa nchi kubwa za Ulaya kama vile Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wametoa matamshi yanayofanana zaidi au kidogo kuunga mkono jibu chanya la Hamas kwa kile kinachoitwa mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Gaza.

Katika jibu lake, harakati hiyo ya muuqawama imesema inakubali “kuwaachilia mateka wote Waisraeli, walio hai na waliopoteza maisha.” Aidha Hamas imeidhinisha “kukabidhi usimamizi wa Ukanda wa Gaza kwa chombo huru cha Wapalestina (wataalamu wa kiufundi) kwa msingi wa makubaliano ya kitaifa ya Wapalestina na kwa msaada wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.”

Hamas imeeleza kuwa jibu lake limetokana na “wajibu wa kitaifa na kwa kuzingatia misingi, haki na maslahi ya juu ya watu wetu.”

Rais wa Marekani Donald Trump alisema Ijumaa jioni kwamba: “Kulingana na taarifa iliyotolewa hivi punde na Hamas, ninaamini wako tayari kwa amani ya kudumu. Israel lazima iache mara moja kushambulia kwa mabomu Gaza ili tuweze kuwaachilia huru mateka hao haraka na kwa amani.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza tamko la Hamas, ambapo msemaji wake Stephane Dujarric amesema kiongozi huyo wa UN “anazitaka pande zote kutumia fursa hii kumaliza mgogoro wa kusikitisha huko Gaza.”

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema ameona jibu la Hamas kwa mpango wa amani kama hatua muhimu ya kusonga mbele. “Tunaunga mkono juhudi za Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye ametuleta karibu na amani kuliko hapo awali,” aliandika kwenye mtandao wa kijamii.

Aidha alisema kuwa, “Sasa kuna fursa ya kumaliza vita, kurudisha wafungwa nyumbani, na kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wale wanaohitaji. Tunatoa wito kwa pande zote kutekeleza makubaliano haya bila kuchelewa.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz pia alitangaza katika ujumbe kwamba kuachiliwa kwa wafungwa na amani ya Gaza iko karibu kufikiwa. Katika katika radiamali yake kwa jibu la Hamas kuhusu mpango wa amani wa Gaza, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X: “Hamas imekubali mpango wa amani wa Rais wa Marekani Donald Trump. Ujerumani inaunga mkono kikamilifu ombi la Rais wa Marekani kwa pande zote mbili. Mateka (wafungwa) lazima waachiliwe.

“Hamas lazima ipokonywe silaha. Vita lazima vikome mara moja. Yote haya lazima yatokee haraka sana,” alisisitiza na kuongeza: “Baada ya karibu miaka miwili, hii ndiyo fursa nzuri zaidi ya amani.”

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia alijibu ripoti za habari za jibu la Hamas kwa pendekezo la Trump kwa kusema kwamba, usitishaji wa mapigano huko Gaza unaweza kufikiwa. “Kuachiliwa wafungwa wote na kusitishwa mapigano huko Gaza kunaweza kufikiwa,” aliandika kwenye akaunti yake ya X (zamani Twitter).

Aliendelea: “Ahadi ya Hamas lazima ifuatiliwe bila kuchelewa. Sasa tuna fursa ya kupiga hatua muhimu kuelekea amani. Ufaransa itatekeleza jukumu lake kikamilifu katika juhudi zake katika Umoja wa Mataifa, pamoja na Marekani, Waisraeli na Wapalestina, na washirika wake wote wa kimataifa.”

Kwa ujumla, madola ya Ulaya yamekaribisha kwa kiasi au kwa muono chanya majibu ya Hamas kwa mpango wa Trump. Ingawa mpango wa Trump una dosari zake, lakini una vipengele, kama vile kuachiliwa wafungwa na kuondolewa vikosi vya Israel kutoka Gaza, ambavyo vinaendana kwa kiasi na misingi ambayo Ulaya inataka.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema, mpango huo wa Trump ni “fursa ya amani ya kudumu” na kwamba umoja huo uko tayari kuunga mkono. Sababu za mwitikio huu wa Ulaya zinaweza kuchunguzwa katika mihimili kadhaa ya kimkakati, kisiasa, kibinadamu na propaganda:

1.       Matumaini ya kumalizika mapigano na kupungua mzozo wa kibinadamu.

Mojawapo ya wasiwasi mkubwa wa serikali za Ulaya na maoni ya umma ni matokeo ya kibinadamu ya vita huko Gaza: Hasara kubwa ya raia, kuhamishwa, shida ya chakula, magonjwa na kusambaratika kwa miundombinu. Wakati Hamas inatoa jibu chanya kwa sehemu ya mpango wa Trump – ikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa mateka na kufanyika mazungumzo – hatua hiyo itaandaa uwanja na mazingira ya kupunguza angalau baadhi ya vitendo vya utumiaji mabavu na kudhibiti madhara ya kibinadamu.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

2.       Mashirikizo ya maoni ya umma na unyeti wa vyombo vya habari

Katika nchi nyingi za Ulaya, vyombo vya habari na maoni ya umma yameathiriwa sana na habari za hali ya Gaza; picha za watoto wasio na makazi, hospitali ambazo haziwezi kuhudumia, na miji chini ya mashambulizi ya anga ya kila siku zinaweka shinikizo kwa serikali kutafuta njia za kupunguza vurugu. Kwa wanasiasa wengi wa Ulaya, hii ni fursa nzuri ya kudai kwamba, wako pamoja na maadili na haki za binadamu, na sio tu maslahi ya watendaji wa utawala. Wakati huo huo, jibu chanya kwa hatua ya Hamas linaweza, kwa kiasi fulani, kupunguza shinikizo la maoni ya umma na kuonyesha kwamba Ulaya iko kwenye njia ya kujaribu kutatua mgogoro huo.

3.       Kuwa tayari kukuumbatia diplomasia na kuupunguza migogoro

Madola ya Ulaya mara nyingi yanapendelea kuchukua nafasi ya upatanishi katika migogoro ya kimataifa. Majibu ya Hamas yasiyo ya moja kwa moja lakini yenye mazungumzo yanaweza kufungua njia kwa Ulaya kuchukua jukumu kubwa zaidi katika mazungumzo. Ikiwa Hamas itaonyesha kwamba imejibu mpango huu si kwa “hapana kabisa” bali kwa “ndiyo kwa masharti au mazungumzo zaidi,” inawezekana kwamba Ulaya itajionyesha kama mpatanishi wa kutegemewa.

4.       Kufungamana na mpango wa “Utatuzi wa madola mawili” na haki za kimataifa

Nchi nyingi za Ulaya zina sera rasmi ya kusisitiza suluhisho la serikali mbili na sheria ya kimataifa. Kwa mtazamo huu, hatua yoyote inayosaidia kupunguza uvamizi, kufikia usitishaji mapigano, kuwaachilia mateka, na kujenga upya maelewano ya kimataifa inachukuliwa kuwa msaada unaohitajika.

5.       Mkakati wa uainishaji mud ana mashinikizo ya natija ya haraka

Huku vita vya Gaza sasa vikiwa vimetimiza miaka miwili na hakuna matokeo ya maana yanayoonekana, mabadiliko yoyote madogo (hata kukubalika kwa sehemu ya mpango wa Trump) yanaweza kuonekana kama hatua nzuri. Kwa kukubali sehemu ya mpango wa Trump bila kuacha muqawama kikamilifu, Hamas inaweza kupata mafanikio (kama vile kuachiliwa kwa mateka au mabadiliko ya namna ya utawala) huku ikihifadhi machaguo yake.

Kwa Ulaya, aina hii ya “harakati ya hatua kwa hatua” inaweza kuwa salama na ya kudhibitiwa zaidi kuliko mabadiliko makubwa na ya haraka; inaruhusu tathmini ya vipengele tofauti na uchanganuzi wa matokeo na kutahmini matukio.

6.       Uwiano katika utendaji kati ya mahusiano na Marekani na maslahi ya kikanda

Ulaya haitaki kujitenga kabisa na mpango wa Marekani; wakati huo huo, kukubaliana nayo kikamilifu kunaweza kuwa na matokeo mabaya katika ulimwengu wa Kiarabu na uhusiano na nchi za Kiislamu. Kukaribishwa kwa tahadhari jibu la Hamas (bila kuunga mkono kikamilifu mpango wa Trump) kunaifanya Ulaya kujiweka katika nafasi ya kidiplomasia yenye akili zaidi; kwani wakati huo huo inaonyesha uaminifu kwa ushiriki wa Marekani katika mchakato wa mazungumzo na wakati huo huo kuleta uwiano kati ya maslahi ya kikanda na haki za binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *