
Kocha Mkuu wa Argentina, Lionel Scaloni ameibua mijadala nchini humo baada ya kumjumuisha kikosini Lautaro Rivero ambaye miaka saba iliyopita alikuwa akifanya biashara ya kutembeza vitu mtaani ‘Mmachinga’ katika mitaa ya jiji la Buenos Aires.
Mchezaji huyo ni miongoni mwa wachezaji 28 walioitwa katika kikosi cha Argentina kwa ajili ya mechi mbili za kimataifa za kirafiki baadaye mwezi huu dhidi ya Venezuela na Puerto Rico.
Beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 21 kabla ya kujiunga na River Plate alikuwa akicheza soka mtaani huku akifanya biashara ya kuuza vitafunwa kwa kutembeza mitaani.
Rivero alikuwa akifanya biashara hiyo kwa lengo la kupata fedha za kusaidia familia yake ya hali ya chini yenye jumla ya watoto watano.
Akiwa na umri wa miaka 14, alionwa na wasaka vipaji wa River Plate ambao walimnyakua na kumuingiza katika kikosi chao cha vijana ambako alionyesha kiwango bora na kufanya mwaka jana apandishwe katika kikosi cha wakubwa.
“Ndoto zangi kubwa zilikuwa kuona familia yangu inaendelea vizuri. Ninataka mama na baba yangu na ndugu zangu wapate kila wanachostahili,” amenukuliwa Rivero katika mahojiano yake na River Plate.
Kikosi hicho cha Argentina kinaundwa na makipa Emiliano Martínez (Aston Villa), Walter Benítez (Crystal Palace) na Gerónimo Rulli (Marseille).
Mabeki ni Cristian Romero (Tottenham), Nicolás Otamendi (Benfica), Nahuel Molina (Atlético Madrid), Gonzalo Montiel (River Plate), Leonardo Balerdi (Marseille), Facundo Cambeses (Racing Club), Nicolás Tagliafico (Lyon), Marcos Acuña (River Plate), Marcos Senesi (Bournemouth) na Lautaro Rivero (River Plate).
Viungo ni Alexis Mac Allister (Liverpool), Enzo Fernández (Chelsea), Leandro Paredes (Boca Juniors), Thiago Almada (Atlético Madrid), Nicolás Paz (Como 1907), Giovani Lo Celso (Real Betis), Rodrigo De Paul (Inter Miami), Franco Mastantuono (Real Madrid) na Aníbal Moreno (Palmeiras).
Washambuliaji ni Giuliano Simeone (Atlético Madrid), Julián Álvarez (Atlético Madrid), Nicolás González (Atlético Madrid), Lionel Messi (Inter Miami), Lautaro Martínez (Inter) na José Manuel López (Palmeiras).