Dar es Salaam. Mwimbaji  wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz kwa sasa anatamba na wimbo mpya, Msumari (2025) ambao kwa mujibu wa ujumbe wake, unaibuka swali  kati yake na mkewe Zuchu nani mtoto?

Wimbo huo uliotayarishwa na Trone, umetoka ukiwa ni takribani miezi minne tangu Diamond kutangaza alishafunga ndoa kimya kimya na Zuchu, mwanamuziki aliyemsaini WCB Wasafi.

Msumari ni wimbo wenye mahadhi ya Bongo Fleva unaozungumzia mapenzi kupitia tungo zilizojaa hisia zikilenga kushinda pambano kati ya upendo wa kweli dhidi ya wivu na wasiwasi wa kusalitiwa. 

Kupitia mashairi mazuri yenye kugusa moyo na kiitikio chenye nguvu, Diamond anamhimiza mpenzi wake (Zuchu) kuupigilia msumari kwa kutumia nyundo ili kuulinda uhusiano wao kwa gharama yoyote ile.

Diamond anauanza wimbo huo kwa kukiri kuwa uhusiano wake wa sasa unapelekea kufanya mambo ya kitoto, anaimba  “Ni utoto tu ila mie kwako sipindui, ndio maana usiku nikinuna najichekesha asubuhi.”

Tunapata picha ya utoto anaozungumzia Diamond kutoka katika wimbo wa Zuchu, Fire (2022) uliotarishwa na Laizer kisha kujumuishwa katika mradi wake, 4:4:2 uliokuwa na nyimbo mbili.

“Akisikia joto, namuogesha, namlaza mapajani, nampepea vizuri. Namrudisha utoto, namnyonyesha, mkubwa ni kwenu ninyi, kwangu hana kauli,” anaimba Zuchu.

Hata hivyo, Zuchu naye kwenye baadhi ya nyimbo zake anajitambulisha kama mtoto kwa mpenzi wake. Nyimbo hizo ni Cheche (2022) na Litawachoma, zote akimshirikisha Diamond, mshindi wa MTV EMAs mara tatu.

“Na bila huruma unanichuuza, mambo unayabaruza. Mi mtoto unanikuza, we haaya,” anaimba Zuchu katika wimbo wa Cheche (2022) chini ya Mocco Genius kutokea studio za Imagination Sound.

Kupitia wimbo wa Litawachoma (2022) uliotayarishwa na Mr. LG, Zuchu anajibu swali lililoulizwa kati yake na Diamond nani mtoto? Jibu tunalipata katikati mwa vesi ya kwanza anaposema; “Nikizidi ugomvi unichape…!”

Na sote unafahamu anayechapwa mara zote ni mtoto.

Ikumbukwe mara baada ya kuachiwa kwa video za nyimbo hizo mbili (Cheche na Litawachoma), ndipo tetesi za Diamond kuwa na uhusiano na Zuchu zilianza kushika kasi mtandaoni ingawa wote walikanusha jambo hilo wakati huo.

Tukirejea katika wimbo huu mpya, Msumari (2025), Diamond anasema. “… ndio maana usipopokea simu siwezagi lala”. Ni wazi Diamond anashindwa kulala kwa sababu anateswa na kumbukumbu nzuri za mapenzi.

Kumbumbuka hizo amezitengeneza akiwa na Zuchu ambaye katika Extended Playlist (EP) yake, I Am Zuchu (2020), kuna wimbo unaitwa ‘Hakuna Kulala’ uliotarishwa na Blaq.

“Namvuta faraghani tumo tubu tubu ndani, namtazama simwishi namkanda mabavuni. Kayainua majeshi vita nichague mimi, aanze Bangladesh amalizie Sudan….. Hakuna kulala, asubuhi itukute,” anaimba Zuchu.

Katika mahojiano na Podcast ya SalamaNa (YahStone Town), Zuchu alisema tangu ameanza muziki huo ndio mstari wake bora zaidi aliowahi kuuandika, na hadi sasa haoni kama kuna wimbo wake unafikia kiwango cha uandishi huo. 

Lakini Zuchu naye hawezi kulala bila mpenzi wake kama anavyoeleza katika wimbo wake, Wana (2020) – “Nikilala naota kama unaniita, nafumba macho navuta shuka, naona napumbazika.”

Diamond anasikia hilo na kujibu kupitia wimbo, Msumari (2025) anaposema; “Lala usingizi upepo wa parizi, mie mambo ya uzinzi aku vya kazi gani…”.

Kupitia ngoma hii mpya, Msumari (2025), Diamond anamtuma njiwa apeleke salamu kuanzia Kivule hadi Lamu kuwa sasa anapendwa. Njiwa anaagizwa apeleke salamu mpaka kwa yule aliyemtesa hapo awali.

Je, kwanini Diamond kamtuma njiwa hadi Lamu, kisiwa kilichopo Pwani ya Kenya? Jibu la swali hilo tunaanza kulichakata katika kolabo yao, Mtasubiri (2022) kutoka katika EP, First of All (FOA) ikitayarishwa na Laizer.

“Oh baby mi mwenzako njiwa wa kufugwa, Oh baby vya chapuchapu vitanifuja,” anaimba Diamond katika wimbo huo. Zuchu naye anajibu. “Oh baby mie wa pwani mzawa wa Unguja, Oh baby penzi laini sitoibuja.”

Hivyo Diamond alimtuma njiwa kwa sababu ni ndege anayempenda kiasi cha kujifananisha naye. Pili, alimtuma kisiwani Lamu akiwa na kumbukumbu nzuri kuwa mpenzi wake wa sasa (Zuchu) pia anatokea kisiwani (Unguja) kama alivyoeleza wenyewe.

Mpenzi huyu alifunga safari kutoka kwao pwani kuja bara ili kuwa karibu na Diamond. Sijasema hivyo kwa utashi wangu, bali maneno ya Zuchu mwenyewe kupitia wimbo wake, Ashua (2020) akimshirikisha Mbosso.

“Upepo wa pwani umenipeleka bara, wewe wangu usukani kwenye penzi barabara,” anaimba Zuchu katika wimbo huo uliotayarishwa na Mocco Genius ambaye naye sasa anaimba Bongofleva.

Na katika kiitikio cha Msumari (2025), Diamond anaposema – “Baby hapo hapo ilipo mbao nigongee, na msumari penzi letu tuboreshe.” Kauli hiyo inaungana na kile alichosema Zuchu katika ngoma, Utaniua (2023); …, “kusepa natoa wapi jeuri. Na kwenye koma kaweka nukta kanitia na kufuli.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *