
Kama unataka kutazama mbashara Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico mwakani unapaswa kuandaa fungu la kutosha ili uweze kumudu gharama za usafiri, malazi na tiketi katika muda utakaokuwepo huko.
Ukiweka kando gharama za huduma za malazi na usafiri ambazo zinatofautiana kutegemea na Shirika la Ndege ambalo shabiki atatumia kutoka nchini mwake kwenda katika nchi hizo au hoteli atakayofikia akiwa huko, gharama za tiketi za kutazama mechi nazo zimechangamka.
Imefichuka kwamba tiketi ya bei ya chini ya kutazama mechi za mashindano hayo itauzwa kiasi cha Dola 60 (Sh147,300).
Bei hiyo ni kwa jukwaa la daraja la nne na ni kwa mechi za hatua ya makundi tu na kwa daraja hilo, gharama ya juu ya tiketi ni Dola 140 (Sh343,700).
Bei ya tiketi katika hatua ya makundi kwa jukwaa la daraja la tatu inaanzia Dola 120 (Sh294,600) hadi Dola 280 (Sh687,400).
Katika hatua ya makundi, tiketi ya Jukwaa la Daraja la Pili itauzwa kati ya Dola 260 (Sh638,300) hadi Dola 605 (Sh1.5 milioni) na tiketi ya Jukwaa la Daraja la Kwanza itauzwa kati ya Dola 345 (Sh846,975) hadi Dola 805 (Sh2 milioni).
Gharama ya chini ya tiketi katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo ambao utaihusisha timu ya Taifa ya Mexico kwa Jukwaa la Daraja la Nne itauzwa kwa Dola 370 (Sh908,350).
Kwa mechi ya ufunguzi ambayo itafanyika Canada ikihusisha timu ya Taifa ya nchi hiyo, gharama ya chini ya tiketi kwa Jukwaa la Daraja la Nne itauzwa kwa kiasi cha Dola 355 (Sh871,525).
Mchezo wa ufunguzi ambao utaihusisha timu ya taifa ya Marekani, tiketi ya bei ya chini zaidi ni Dola 560 (Sh1.4 milioni).
Tiketi ya bei ya juu zaidi katika Fainali za Kombe la Dunia ni ya Jukwaa la Daraja la Kwanza katika mechi ya fainali ambayo itauzwa kiasi cha Dola 6,370 (Sh16 milioni).
Mchanganuo wa gharama za tiketi kombe la dunia 2026
Daraja 1 Daraja 2 Daraja 3 Daraja 4
Ufunguzi Mexico Sh4.5 mil Sh3 mil Sh1.8 mil Sh907,710
Ufunguzi Canada Sh4 mil Sh3 mil Sh1.8 mil Sh870,911
Ufunguzi Marekani Sh7 mil Sh4.8 mil Sh2.7 mil Sh1.2 mil
Hatua ya Makundi Sh846,378 Sh637,850 Sh294,392 Sh147,182
Mshindi wa Tatu Sh2.5 mil Sh1.8 mil Sh883,177 Sh404,789
Fainali Sh16 mil Sh10 mil Sh6.9 mil Sh4.5 mil