
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia na Rais wa Yanga, Hersi Said wameteuliwa katika kamati tofauti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Karia ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Kamati ya FIFA ya Soka la Ufukweni.
Wakati Karia akilamba uteuzi huo, Hersi ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Klabu za Soka za Wanaume Duniani.
Ikumbukwe kwamba Hersi ni Mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA).
Uteuzi huo wa Karia na Hersi utadumu kwa muda wa miaka minne kuanzia 2025/2029.
Uteuzi huo haujaishia kwa Karia na Hersi tu kwa upande wa Afrika Mashariki kwani hata Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF), Hussein Mohammed naye ameupata.
Mohammed ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Mahusiano ya Kitaasisi wa FIFA.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino na kupitishwa na Baraza la Shirikisho hilo.