Huenda ule utatu wa MLS unaomaanisha nyota watatu wa soka duniani, Lionel Messi, Neymar na Luis Suarez ukaanza kuonekana nchini Marekani siku chache zijazo baada ya kutokuwa pamoja kwa muda mrefu.
Hiyo ni kufuatia timu ya Inter Miami inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani kuanza harakati za kumnasa Neymar anayeitumikia Santos ya Brazil.
Uongozi unaomsimamia Neymar unaripotiwa umeitaarifu Inter Miami kuwa inaweza kumnasa Neymar katika dirisha dogo la usajili la majira ya baridi.
Neymar alijiunga na Santos ambayo ni klabu yake ya utotoni mwezi Januari mwaka huu kwa mkataba wa miezi sita baada ya mkataba wake na Al Ittihad ya Saudi Arabia kuvunjwa.
Baadaye alisaini mkataba wa kuitumikia Santos kwa miezi mingine sita ambao utafikia tamati Desemba mwaka huu hivyo kwa sasa, kanuni zinamruhusu kufanya makubaliano na klabu nyingine kwa vile mkataba uko chini ya muda wa miezi sita.
Inaonekana kama Neymar ni usajili wa kimkakati kwa Inter Miami baada ya timu hiyo kuwapoteza nyota wengine wawili wa zamani wa Barcelona, Sergio Busquets na Jordi Alba ambao wamestaafu kucheza soka.
Taayari timu hiyo imeshamnasa beki wa zamani wa kushoto wa Tottenham Hotspur, Sergio Reguilon lakini pia ina nyota inaowasaka kutoka barani Ulaya na sasa imemuongeza Neymar katika vipaumbele vyake vya usajili.
Wakati ikianza kuiwinda saini ya Neymar, timu hiyo pia kwa sasa ipo katika meza ya mazungumzo na Messi (38) na Suarez (38) kwa ajili ya kuwaongezea mikataba ya kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Ingawa makubaliano bado hayajaanza, wawakilishi wa Neymar wanatambua thamani kubwa ya nje na ndani ya uwanja ambayo Neymar atapata kwa kwenda kucheza soka la kulipwa Marekani katika mwaka ambao Kombe la Dunia 2026 litafanyika.
Upande wa Neymar unaiona Ligi Kuu ya Marekani kama sehemu sahihi ambayo itamfanya mshambuliaji huyo kurudisha makali yake ambayo kwa sasa yanaonekana kushuka.
Wakati Messi, Suarez na Neymar wakicheza pamoja katika kikosi cha Barcelona kati ya 2014-2017, kwa pamoja walifunga mabao 364 na kupiga pasi za mwisho 173.