
Marekani. Mwigizaji na mwimbaji maarufu kutokea Marekani, Jennifer Lopez (J.Lo), 56, amesema alishiriki mashindano ya triathlon ikiwa ni miezi sita baada ya kujifungua mapacha wake, Emme na Max, 17.
Mkali huyo wa kibao, Ain’t Your Mama (2016), ameeleza kuwa jambo hilo lilimpa nguvu na motisha kubwa ya kuurudisha mwili wake katika hali ya kawaida baada ya ujauzito.
Triathlon ni mashindano yenye mchanganyiko wa michezo mitatu mfululizo ambayo ni kuogelea, kuendesha baiskeli na kukimbia, huku mchezaji akitakiwa kufanya yote bila kupumzika.
Umbali na muda hutegemea ila ni mchezo unaohitaji nguvu, uvumilivu, pamoja na maandalizi ya hali ya juu ya mwili na akili kwa mshiriki.
Akizungumza katika kipindi cha Las Culturistas Podcast kilichorushwa hewani Jumatano, Oktoba 8, Lopez alielezea jinsi alivyopanga kushiriki mashindano hayo akiwa bado mjamzito.
“Wakati nikiwa mjamzito, nilijiambia nitashiriki triathlon baada ya kujifungua ili kurudisha vizuri tumbo langu. Nilijiwekea lengo hilo,” alisema Lopez.
Alisema alihamasishwa na kipindi cha televisheni, na alipofanya utafiti, aligundua kuwa kungekuwa na mashindano ya triathlon mjini Malibu mnamo Septemba 2008. Msukumo wa kutaka kufanya hivyo ni ili watoto wake wawe na kitu cha kujivunia.
“Nilitaka watoto wangu wajivunie mimi. Niliona tuzo yangu ya American Music Award 2007 na nikafikiria, ‘hili ni jambo zuri kwao kujivunia.’ Ndio maana nikaamua kushiriki triathlon,” alisema.
“Sasa, nikiwaambia hadithi hiyo. Hawajali kabisa. Ni kama vile, ‘Sawa, ulishiriki triathlon.’ Lakini labda siku moja watakumbuka na kusema, ‘Wow, mama yangu alishiriki triathlon miezi sita tu baada ya kunizaa,” alieleza.
Hata hivyo, Lopez alifichua kuwa licha ya kushiriki mashindano hayo kwa mafanikio, sehemu ya kuogelea ilimpa changamoto kubwa.
“Kuogelea ndio sehemu ya kutisha zaidi. Unaangalia bahari na unaambiwa uogelee hadi ufikie boya la tatu. Basi nilijisemea labda kuna papa huko,” aliongeza kwa utani.
Pia alielezea jinsi alivyochukua uamuzi wa kupumzika mwaka mzima ili kuwa karibu na watoto wake baada ya miaka mingi ya kufanya kazi mfululizo katika kiwanda cha muziki na filamu.
“Mwaka jana nililazimika kufuta ziara yangu na nikachukua mwaka mzima kupumzika. Nilikaa nyumbani na watoto wangu, tulirejesha ukaribu wetu. Ilikuwa hisia nzuri sana kwao na kwangu pia,” alisema.
Watoto hao, Emme na Max, mapema waliongozana na mama yao huko New York katika uzinduzi wa filamu, Kiss of the Spider Woman (2025) ambayo Lopez kashiriki kuiandaa na kuigiza.
Ikumbukwe Jennifer Lopez alijaliwa watoto hao Februari 22, 2008, wakati huo bado alikuwa katika ndoa yake na mwanamuziki Marc Anthony, 57, ambaye inaripotiwa uhusiano wao ulianza mwishoni mwa miaka ya 1990.
Mastaa hao walifunga ndoa Juni 5, 2004, na kutangaza kutengana Aprili 9, 2012 ingawa shauri la talaka yao lilikamilishwa Juni 16, 2014, huku Lopez akihifadhi haki ya msingi ya kuwalea watoto, kwa mujibu wa mahakama.