
Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetangaza kifo cha mwanachama wake, Daniel Mbega, aliyefariki dunia leo Jumamosi, Oktoba 11, 2025, katika Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, imeeleza kuwa kwa mujibu wa familia, Mbega alizidiwa majira ya saa 10 alfajiri na alikimbizwa Hospitali ya Temeke kwa matibabu, ambako alifariki dunia wakati madaktari wakiendelea kumhudumia.
“Daniel Mbega alikuwa mwandishi wa habari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20, hasa katika uandishi wa habari za uchunguzi. Ameshafanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari na kuchangia pakubwa kukuza tasnia ya habari nchini,” amesema Balile katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mbega alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chigwingwili, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, kisha akaendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Pugu. Baadaye alisomea uandishi wa habari katika Chuo cha Tanzania School of Journalism (TSJ).
Taarifa hiyo imeongeza kuwa hadi mauti yanamfika, Mbega alikuwa mwanachama hai wa TEF, akitambulika kwa mchango wake wa kitaaluma, nidhamu ya kazi na kujitolea kuendeleza misingi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa kesho, Jumapili Oktoba 12, 2025, katika Hospitali ya Temeke kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwao Chigwingwili, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu.
“TEF inaungana na familia, ndugu, jamaa, marafiki na wanahabari wote nchini katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Tunatoa pole za dhati kwa familia ya marehemu na tunamuombea apumzike kwa amani,” imesema taarifa hiyo.