
Dar es Salaam. Ukifika mwezi Desemba, kuna vibe ambalo halihitaji tangazo la serikali. Halihitaji sauti ya mkuu wa kimila wala ukoo. Huu mwezi dunia nzima inaweka shida chini na kuweka mikono juu. Kisha ni kubanjuka tu.
Hata kama huna kalenda, mwili wenyewe unajua. Ni msimu wa Xmass na mwaka mpya! Hata hali ya hewa ‘inachenji’. Ni muziki kila kona, maduka hushusha bei, ni mwendo wa kupiga ndulu za mwisho wa mwaka.
Acha upimbi kama hujui, tambua maandalizi ya Desemba huanza Novemba. Wengine wanatafuta ‘lokesheni’ ya kufungia mwaka. Wengine hutengeneza bajeti ya pamba za kufa mtu.
Wapo wale wanapangia washikaji “get together” ya kistaa. Kwenye mitandao, utaona maneno kama “December loading!” au “Vibes only this season.” Unyama flan wa kufuta wazo la uwepo wa kifo.
Ni kama vile akili zetu zinahama. Kutoka kazini kunata na ‘mode’ ya bata! Na cha kufurahisha, hata wale ambao mwaka uliwaendea vibaya, nao hupata matumaini mapya. Ni mwezi wa tabasamu.
Na moyo wa Xmass una kitu cha kipekee. Unaleta amani, upendo, na ile hisia ya “Ah, ‘gaiizi’ tumefika salama.” Kina Macha, Urio, Tesha, Ngowi, Tarimo, Minjaeli, Masawe, Kilema na Meku. Akili ipo ‘kihomu switi homu’ kuhesabiwa.
Desemba bila muziki ni sawa na chapati bila maziwa! Mitaani, kila kona kuna spika inazungumza. Ni Singeli, Amapiano, Bongo Fleva, na Kiduku. Yote inasukumwa kwa nguvu kwa kunogeshwa na tungi.
Wengine wanatengeneza ‘pleilisti’ mapema kwa ajili ya ‘hausi pati’ au ‘rodi tripu’. Hata wanaosema hawatoki, msimu huu utasikia wakisema, “basi twende kidogo tu.” Kubaki ndani kama utumbo ni usolo na uboya.
Kwa vijana wengi, huu ndio muda wa kupumua baada ya stress za mwaka mzima. Kama kazi, shule au maisha yalibana, Desemba ni ‘taim’ ya kusahau presha, kucheka na kuishi. Waebrania huita mwezi wa kuongeza umri.
Hapo ndipo mchezo unabadilika! Wengine wana “mpango” lakini hakuna “budget.” Mishahara ya mwisho wa mwaka inasubiriwa kama matokeo ya NECTA. Baba usiombe uingie Desemba ukiwa na misala ya mkwanja.
Kuna sisi ambao hela inakuja na kupotea kwa siku moja tu. ‘Autfiti’ ya Xmas inameza kila kitu. Huna unachobakiwa nacho mwilini na akilini zaidi ya ule mning’inio wa tungi. Gen Z wanaita ‘Mishahara Haikutani.
Januari ikifika ni msala kinomaa. Simu zinanyamazishwa, marafiki hawapokei. Kila mtu anaandika ‘statasi’ “Mwaka mpya, sina kosa jipya.” Kuna jumbe nyingi zile za kisolo kwa mtindo wa ‘memezi’.
Lakini ukweli ni kwamba, vijana wengi wanajua jinsi ya kuishi kwa muda. Wanasema, “kufa kisanaa bora kuishi kistaarabu.” Wengine wanaweka akiba ndogo, wengine wanajipanga kuanzisha kitu kipya mwaka unaofuata.
Xmass bila penzi kama pilau bila nyama. Ni msimu wa “matching outfits,” couple goals, na soft life pictures kwenye Insta. Wa kutoka out, kwenda beach, mbugani na wale wa kuchoma nyama kitaani.
Kila mtu anataka kumbukumbu na caption lazima iwe kali. Lakini pia, msimu huu ni wa maridhiano.
Wale waliokuwa wamegombana, hutuma DM ya “Happy holidays.” Unyamwezi tu. Wengine wanarudiana, wengine wanatulia, wengine hukubaliana kuanza upya mwaka unaofuata.
Ni msimu wa moyo kuufanya uwe mwepesi na furaha kuwa rahisi. Hakunaga wakati amazing kama Desemba.
Kila mwisho wa mwaka, vijana wanapenda kuandika resolutions. Wengine husema: “Mwaka ujao lazima nihame kwa mama,” Ama “Naacha pombe, naanza gym,”au “Naenda kusoma, au kuanza biashara.”
Hata kama baadhi hawatekelezi yote, bado ni hatua ya matumaini. Mwaka mpya huja na nguvu mpya na ari mpya. Waswahili wa Iringa husema, usiye na matumaini ni maiti inayotembea. Binadamu ni lazima uwe na tumaini.
Na usisahau, Desemba ni muda wa familia pia. Kuna vijana wengi wanaorudi nyumbani kwa wazazi. Wanaenda kijijini, wanakutana na ndugu, wanakumbuka walikotoka.
Ni kipindi cha kujipanga, kujipima, na kuanza upya kwa tabasamu. Kifupi, Xmass na Mwaka Mpya, kwa vijana ni mchanganyiko wa bata, matumaini na maisha halisi.
Ni muda wa kuachilia presha na kujipanga upya, kuanza mwaka mpya na roho safi. Usivuke na kinyongo. Lakini ujumbe muhimu unabaki uleule: Bata kwa akili na starehe kwa mpangilio. Usisahau Januari nao ni mwezi! Na huwezi kufika Desemba bila kuanza na January, na huwezi kumaliza Desemba bila kupita January.
So! Bata iwe na baraka! Huu ndo wakati wa kutunza pesa za vibe la Desemba. ‘Everi singo senti’ tunza na kuificha mbali na macho yako ya uzinzi na ulevi. Xmass kuila kwa macho ni upimbi. Jibane leo kesho ukatishe.