Dar es Salaam. Aliyekuwa mwanamuziki wa Konde Music Worldwide kwa takribani miaka mitano, Ibraah ameachia wimbo wake wa nne (Bei Chei) tangu alipoachana na lebo hiyo inayomilikiwa na Harmonize mnamo Mei.
Katika kuutangaza wimbo huo kupitia mahojiano mbalimbali na redio na mitandao, Ibraah amekuwa akitupa lawama kwa Konde Music kwa madai kuna sehemu hawakuwajibika ipasavyo!.
Moja ya madai hayo ni kwamba nyimbo zake nyingi hazikutoka kwa wakati na hata baadhi ya video zake hazikufanyika kwa kiwango kinachohitajika huku Boss (Harmonize) akiachia mfululizo wa kazi.
Lakini madai haya yana ukweli kiasi gani?, au Ibraah anataka kuchangamsha genge ili kupata huruma ya mashabiki?
Ikumbukwe Harmonize alitangaza kufungua Konde Music hapo Oktoba 10, 2019, muda mfupi tangu kuachana na WCB Wasafi yake Diamond Platnumz. Na kufikia Aprili 11, 2020, Konde Music wakamtamulisha Ibraah.
Akiwa kama msanii wa kwanza chini ya Konde Music, Ibraah alitambulisha na Extended Playlist (EP) yake, Steps (2020) yenye nyimbo tano, huku akiwashirikisha Harmonize pamoja na Joeboy na Skiibii, wote kutokea Nigeria.
Moja ya nyimbo za EP hiyo, ni ‘One Night Stand’ aliomshirikisha Harmonize, ulifanya vizuri hadi mwishoni mwa 2020 video yake ilishika nafasi ya nane katika orodha ya ngoma za Bongofleva zilizofanya vizuri YouTube.
Hata hivyo, video hiyo ilianza kuleta mashaka kuhusu wawili hao, sababu ni kwamba wimbo ni wa Ibraah lakini video ikawekwa katika chaneli ya YouTube yake Harmonize!.
Mashabiki wakajiuliza mbona kolabo za Harmonize akiwa na WCB Wasafi Diamond hakufanya kitu kama hicho?, au Harmonize ana wasiwasi na Ibraah kuwa kuna siku atamgeuka?
Ndivyo ilivyokuja kuwa mnamo Mei 2025, Ibraah alipoamua kuachana na Konde Music akiwa ni msanii mwisho kufanya hivyo baada ya Country Wizzy, Cheed, Killy na Anjela.
Itakumbukwa hadi anaondoka Konde Music, Ibraah alikuwa ameshirikiana na Harmonize katika nyimbo – One Night Stand (2020), Addiction (2021), Mdomo (2022), Tunapendeza (2023) na Dharua (2024).
Nyimbo zote hizo video zake zimetoka na kufanya vizuri, mathalani wimbo ‘Dharua’ imeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 28 ikiwa ndio video ya Ibraah yenye namba nyingi katika mtandao huo.
Hivyo ni wazi Harmonize alifanya kazi kubwa kwa Ibraah na sio kwa udogo huo kama mwanamuziki huyo anavyotaka ionekane katika mfululizo wa mahojiano anayofanya kwa sasa.
Chini ya lebo hiyo, Ibraah alitoa EP nne, Steps (2020), Karata 3 (2021), Air Piano (2024) na Love Season(2025) pamoja na albamu moja, The King of New School (2022).
Ndiye msanii pekee aliyetoa EP nyingi chini ya lebo hiyo, na pia msanii pekee aliyeweza kutoa albamu. Wenzake wote walitoa EP moja moja, na wengine hadi wanaondoka hawakupata hata hiyo EP moja sembuse albamu.
Albamu yake ina nyimbo 17 na kuwashirikisha Maud Elka, Christian Bella, L.A.X, Waje, AV, Roberto na Bracket. Kama sio Konde Music, ni wazi ingekuwa ngumu kwake kuwashirikisha wasanii hao hasa Maud Elka na Joeboy aliyesika katika EP ya kwanza.
EP zote na albamu zina nyimbo 32, na kwa ujumla Ibraah alitoa nyimbo zaidi ya 50 ndani ya miaka yake mitano chini ya Konde Music, ikiwa ni wastani wa nyimbo 10 kila mwaka.
Hivyo madai ya nyimbo zake kucheleweshwa kwa kiasi yanakosa nguvu labda kuna jingine nyuma ya pazi ambalo hajataka kuliweka wazi.
Tunafahamu mwaka 2023 alisuasua kidogo ila yeye pamoja na lebo walidai kuna kampuni ya usambazaji muziki kidijitali ndio iliyokuwa inawachelewesha pamoja kushikilia malipo ya kazi zao ila baadaye mambo yalionekana kuwa sawa.
Kwa mujibu wa Ibraah, yeye alikuwa akiuza CD za nyimbo mtaani, aliposikia Harmonize amefungua lebo akaanza kusaka nafasi hiyo hadi akakutana na aliyekuwa mtayarishaji wa Harmonize, Bonga.
Bonga alivutiwa na uwezo wake ila akamshauri akarekodi hata wimbo mmoja. Kazi aliyorekodi ikachukuliwa na DJ Seven na kupelekwa kwa Harmonize ambaye aliona kipaji chake na kuamua kumsaini Konde Music.