Karatu. Utafiti unaoendelea katika Bonde la Eyasi Wembere, unaolenga kubaini uwepo wa mafuta na gesi asilia, umeonesha matumaini makubwa ya kupatikana kwa nishati hizo muhimu nchini.

Akizungumza leo Oktoba 10, 2025 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utafiti huo wilayani Karatu, mkoani Arusha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio, amesema matokeo ya awali yanaonyesha uwepo wa miamba yenye sifa za kuhifadhi mafuta katika bonde hilo.

“Kazi za utafiti zilianza mwaka 2015 ambapo tumekuwa tukikusanya data mbalimbali zinazohusiana na uwepo wa mafuta na gesi. Baada ya uchambuzi wa data hizo, tumebaini kuwa eneo hili lina miamba ambayo inaweza kuhifadhi mafuta,” amesema Dk Mataragio.

Amefafanua kuwa awamu ya kwanza ya utafiti ilihusisha uchunguzi wa anga na uchorongaji wa visima vifupi, uliogharimu takribani Sh8 bilioni, huku utafiti wa mitetemo (seismic) wa kilomita 260 ukigharimu Sh10 bilioni.

Kwa mujibu wa Dk Mataragio, amesema awamu ya pili ya utafiti inahusisha eneo lenye urefu wa kilomita 914 na inatarajiwa kugharimu Sh43 bilioni, ambapo hadi sasa asilimia 47 ya kazi imekamilika sawa na kilomita 430.

“Tunatarajia kukamilisha awamu ya pili kufikia Aprili 2026. Nimeagiza kazi ziendelee hata kipindi cha mvua ili mradi usichelewe,” ameongeza.

Amesema iwapo mafuta yatapatikana, Tanzania itanufaika kwa kupunguza gharama za kuagiza mafuta kutoka nje na hivyo kutunza akiba ya fedha za kigeni.

Dk Mataragio pia amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa mradi huo, asilimia 90 ya watendaji ni Watanzania, jambo alilolitaja kuwa ni mafanikio katika kujenga uwezo wa kitaifa katika sekta ya utafutaji mafuta na gesi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi kutoka TPDC, Mjiolojia Paschal Njiko, amesema shirika hilo linashirikiana na kampuni ya African Geographical Services (AGS), ambayo ni mkandarasi mzawa, katika kutekeleza utafiti huo.

“Tumezingatia maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu na tutaendelea kumsimamia mkandarasi kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati,” amesema Njiko.

Naye, Mwenyekiti wa AGS, Salum Haji, ameahidi kukamilisha kazi kwa wakati na kwa ubora unaohitajika, akisema wanatambua umuhimu wa mradi huo kwa taifa.

Mmoja wa vijana walionufaika na ajira kupitia mradi huo, Biru Benjamini, amesema mradi huo umeleta fursa za ajira na mafunzo kwa vijana waliokuwa hawana kazi.

“Kupitia mradi huu sisi vijana tumenufaika na ajira na kupata ujuzi wa kazi za utafiti,” amesema Benjamini.

Mradi wa Bonde la Eyasi Wembere ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya Serikali inayotekelezwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa lengo la kuongeza uwezo wa nchi katika kugundua na kutumia rasilimali za mafuta na gesi asilia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *