Barcelona imeanza kuitega Man United katika dili la mshambuliaji Marcus Rashford aliyetua klabuni hapo kwa mkopo wakati wa usajili wa majira ya kiangazi, baada ya kuonyesha nia ya kumsajili moja kwa moja.

Vigogo hao wa Catalonia, wamevutiwa na bidii na kipaji cha mshambuliaji huyo wa England tangu alipojiunga na timu hiyo kutoka Old Trafford.

Rashford mwenye umri wa miaka 27, ambaye kwa sasa yuko kwenye kikosi cha England kinachojiandaa na mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Latvia Oktoba 14, 2025, tayari ameifungia Barca mabao matatu na kutoa pasi za mabao tano katika mechi kumi msimu huu 2025-2026.

Kiwango chake kimewafurahisha sana mabosi wa klabu hiyo, ambao awali walihofia huenda kulikuwa na tatizo kati yao na Rashford kwa Man United, lakini wamebaini bado ana uwezo mkubwa na hakuna tatizo ambalo lingeweza kumharibia soka lake.

RASH 01

Chanzo kutoka Barcelona kimesema: “Barcelona ilikuwa na wasiwasi kumsajili Marcus mwanzoni mwa msimu huu, hasa kutokana na hali ya kifedha ya klabu.

“Lakini pia walihisi huenda Man United walikuwa wanaficha jambo, walishangaa kwa nini waliamua kumwachia mchezaji kama huyo kirahisi.

“Walidhamiria kulichunguza zaidi suala hilo. Dwaine, kaka yake Marcus, aliwahakikishia kuwa hakuna tatizo lolote, na ndugu yake hakuwa mtu wa kuwaingiza mkenge.”

Kwa sasa Barca wanaendelea kushangazwa na mshambuliaji huyo kwa kuonyesha soka safi na lenye ushindani ambalo linaisadia klabu hiyo katika kampeni zake za kutetea taji la La Liga msimu huu 2025-2026.

Kwa mujibu wa SunSport, Barcelona watalazimika kulipa Pauni 25 milioni, ili kumsajili rasmi Rashford, pamoja na nyongeza ya Pauni 5 milioni huku Man United wakitarajiwa kupata asilimia fulani ya ada iwapo atauzwa tena siku za usoni.

Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, pia amefichua kuwa majira ya joto yaliyopita alimsihi mkurugenzi wa michezo Deco kumsajili Rashford.

Flick amesema: “Nilimwambia Deco majira ya joto, ‘Niletee Rashford, tafadhali, niletee Rashford’. Tulihitaji mchezaji wa aina yake.”

Licha ya mechi ya kwanza ya kuwavunja moyo mashabiki wa Barcelona, Rashford aling’ara katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Newcastle, akifunga mabao mawili.

RASH 02

Baada ya mchezo huo, Flick alisema alifurahia sana juhudi za mshambuliaji huyo na kwamba mabao aliyoyafunga kwenye mechi hiyo, yalimpa Rashford kujiamini zaidi.

Rashford pia amemvutia kocha wa England, Thomas Tuchel, na aliingia kipindi cha pili katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wales, kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa Wembley, Oktoba 9, 2025, huku akitarajiwa kuanza katika mechi ya Oktoba 14, 2025 dhidi ya Latvia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *