Nyota wa Chelsea, Enzo Fernandez, amerejea jijini London, kufuatia hofu ya kuwa na majeraha ambayo huenda yakamuweka nje ya uwanja kwa siku kadhaa.
Kiungo huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha Argentina kilichoitwa wiki iliyopita kwa ajili ua michezo ya kimataifa ya kirafiki.
Enzo alicheza dhidi ya Venezuela Oktoba 10, 2025, lakini mashabiki wengi walishangaa kuona hakuwa kwenye kiwango chake cha kawaida.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka GOAL, Fernandez anasumbuliwa na maumivu kwenye goti lake la kulia, ambapo alipokuwa kambini na Argentina, alionekana akiwa amefunga bandeji kwenye wakati wa mazoezi.
Licha ya hali hiyo, aliweza kucheza dakika 78 katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Venezuela kwenye Uwanja wa Hard Rock juzi.
Fernandez anatarajiwa kufanyiwa vipimo jijini London, ili kubaini ukubwa wa jeraha lake, ambalo limeanza kuzua hofu kwa kocha Enzo Maresca anayehitaji kumtumia kwenye mechi itakayowakabili baada ya kalenda ya FIFA.
Fernandez amekuwa mchezaji muhimu kwa Chelsea msimu huu, akichangia mabao matatu na asisti moja katika mechi 10 kwenye mashindano yote aliyocheza.
Hata hivyo, Chelsea tayari inakumbwa na wimbi la wachezaji majeruhi kama Tosin Adarabioyo, Levi Colwill, Liam Delap na Wesley Fofana.
Chelsea ilimsajili Enzo Fernandez kutoka Benfica kwa ada inayokadiriwa kuwa Pauni 105 milioni, Januari 2023. Tangu wakati huo, ameifungia Chelsea mabao 19 na kutoa asisti 24 katika mechi 125 alizocheza.