Dar es Salaam. JKT Queens imebeba taji la Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuifunga Simba Queens mabao 2-1, kwenye mchezo mkali uliopigwa katika Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Hii ina maana kuwa sasa JKT ndiyo wababe wa michuano hiyo iliyofanyika kwa mwaka wa tatu, ikiwa imetwaa ubingwa huo mara mbili huku Simba ikitwaa mara moja.
Timu hiyo imeonyesha umwamba baada ya kutwaa ubingwa huo kwa kuzifunga timu zote kubwa, ilianza kwa kuifunga Yanga Princess kwa penalti 6-5 baada ya sare dakika tisini za mchezo na jana ikaifunga Simba Queens kuonyesha kuwa ipo tayari kwa ajili ya Ligi Kuu inayoanza Novemba sita.
Bao la Winfrida Gerald dakika ya 12 na lile la Simba walilojifunga la winga Asha Omary dakika ya 17 liliipa timu hiyo taji la pili la mashindano hayo na lile la kufutia machozi la Wanamsimbazi likifungwa na Zawadi Usanase mwishoni mwa mchezo.
Winga wa JKT Winifrida amekuwa msumari wa moto kwa vigogo Simba Queens na Yanga Princess akiwafunga wote wawili kuanzia nusu fainali na leo fainali ambapo alitangazwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo.
Katika mechi ya leo Winifrida ameonyesha kiwango bora akiwapita mabeki wa Simba na kumchezea faulo nyingi ambazo zilikuwa na faida kwa Wanajeshi hao.
JKT ilionekana kucheza kwa kuelewana hasa eneo la kiungo wakianza kutengeneza mashambulizi kutokea chini hadi kwa mawinga wake.
Hata hivyo, Simba ambayo takribani wachezaji watano kati ya 11 walioanza walikuwa wapya hivyo walionekana kukosa muunganiko.
Katika mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu, Yanga Princess iliichapa Mashujaa Queens mabao 3-0 kwenye uwanja huohuo, mchezo ulioanza saa 6:00 mchana.
Yanga chini ya Kocha Edna Lema ‘Mourinho’ ilicheza mechi hiyo baada ya kutolewa hatua ya nusu fainali na JKT Queens.
Timu hiyo ilionyesha kiwango bora tangu dakika za mwanzo, ikimiliki mpira na kushambulia kwa kasi kupitia viungo wake wa pembeni.
Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 16 na Jeanine Mukandayisenga aliyemalizia krosi ya Precious Christopher baada ya ukuta wa Mashujaa Queens kujichanganya, staa huyo ambaye amekuwa bora kwenye mashindano hayo ndiye ametangazwa kuwa mfungaji bora wa mashindano hayo mwaka huu.
Dakika ya 48 Precious aliiongezea la pili akimalizia pasi ya Mukandayisenga na dakika 18 baadaye Aregash Kalsa akaweka kambani bao la tatu kwa asisti ya Adebis Ameerat.
Katika mchezo wa leo, Edna alifanya mabadiliko kwenye maeneo matatu, eneo la golikipa akianza na Ester Emily aliyechukua nafasi ya Zubeda Mgunda aliyeanza mechi ya nusu fainali, kiungo akianza Adebis Ameerat aliyempisha Agnes Pallangyo aliyeanzia benchini.
Eneo jingine la beki wa kushoto alianza Protasia Mbunda baada ya Wincate Kaari kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi iliyotangulia na upande wa kulia alicheza Diana Mnally akichukua nafasi ya Wema Maile ambaye hakuwapo kabisa kwenye benchi.