Guinea ya Ikweta, imemfuta kazi kocha wao Juan Micha na kuwaondoa baadhi ya wachezaji muhimu kikosini baada ya mgomo uliosababisha timu hiyo kushindwa kusafiri kwenda Malawi kwa ajili ya mechi ya kufuzu Kombe la Dunia, jambo linaloweza kuiweka nchi hiyo kwenye hatari ya kuadhibiwa na Shirikisho la Mpira wa Kimataifa (FIFA).
Taarifa zinasema wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza, akiwemo nahodha mkongwe Emilio Nsue, wameondolewa kwenye timu kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Kundi H dhidi ya Liberia unaotarajiwa kuchezwa kesho Jumatatu Oktoba 13, 2025.
Wachezaji hao waligoma kusafiri kwa ajili ya mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 iliyopangwa kufanyika Alhamisi Oktoba 9, 2025 wakilalamikia hali duni na kutolipwa fedha zao, jambo lililopelekea kocha pamoja na baadhi ya wachezaji kufukuzwa kutoka kwenye kikosi.
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Guinea ya Ikweta limethibitisha kufutwa kazi kwa Micha kupitia ukurasa wao wa mitandao ya kijamii.
“Tume ya Michezo imewapa fursa wachezaji walioitwa kwa mechi hizi za FIFA ambao bado wanataka kulitumikia taifa lao kujiandikisha majina yao kwenye orodha mpya ya kukumbukwa,” imesomeka taarifa hiyo.
“Iwapo mtu hatofanya hivyo, atachukuliwa kwamba amejiondoa mwenyewe na hatakuwa tena sehemu ya timu ya taifa.”
Timu mpya tayari imetangazwa kwa ajili ya mchezo wa Jumatatu, huku Casto Nopo akiteuliwa kuwa kocha wa muda.
Orodha hiyo haijajumuisha wachezaji wengi waliokuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kilichopita, ambapo Guinea ya Ikweta ilishtua ulimwengu kwa kuifunga wenyeji Ivory Coast mabao 4–0 katika hatua ya makundi, matokeo yaliyotajwa kuwa moja ya mshangao mkubwa zaidi katika historia ya michuano hiyo.
Timu hiyo pia ilitoka sare ya 1–1 na Nigeria katika mechi ya kwanza ya mashindano hayo mapema mwaka 2024, na kuongoza kundi lao mbele ya vigogo hao wawili kabla ya kutolewa katika hatua ya 16 bora na Guinea kwa bao la dakika za mwisho.
Tangu wakati huo, Guinea ya Ikweta tayari imefuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 lakini wameondolewa kwenye mbio za kufuzu Kombe la Dunia 2026.