Manchester, England. Harry Maguire yuko tayari kukataa ofa ya mshahara wa pauni 500,000 kwa wiki kutoka Saudi Arabia ili kusaini mkataba mpya na Manchester United, kwa mujibu wa ripoti.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 32 anatarajiwa kuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu huu, na tayari amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa kutoka Mashariki ya Kati.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa England alipata umaarufu mkubwa chini ya kocha Ruben Amorim msimu uliopita, lakini msimu huu ameanza mara mbili tu katika Ligi Kuu ya England.
Iwapo angeamua kuhamia Saudi Arabia, Maguire angepokea malipo makubwa mno, huku klabu za Al-Nassr ya Cristiano Ronaldo na Al-Ettifaq zikisemekana kuwa na nia ya kumsajili.
Hata hivyo, gazeti la Mirror linaripoti kuwa Maguire yuko tayari kukataa ofa hiyo ya kifahari na kujitolea kuendelea kusalia Old Trafford, iwapo klabu hiyo itamwongezea mkataba.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa Maguire anafahamu kwamba kujiunga na klabu ya Saudi Arabia kunaweza kuathiri nafasi yake ya kuitwa tena kwenye timu ya taifa ya England chini ya kocha Thomas Tuchel.
Maguire alijiunga na United kutoka Leicester City kwa pauni milioni 80 mwaka 2019 ada ambayo bado ni rekodi ya usajili wa beki hadi sasa.
Tangu wakati huo, ameichezea United mara 253, na mwezi uliopita alitunukiwa fremu maalum kutoka kwa Mkurugenzi wa Soka, Jason Wilcox, kuadhimisha mechi yake ya 250 akiwa na klabu hiyo.